Sikia Jackson alichoifanyia Bayern Munich
Muktasari:
- Kwa mujibu wa ripoti kutoka Ujerumani, Jackson alikataa sehemu ya pesa aliyopewa na Bayern kama bonasi ya usajili ili kuhakikisha anajiunga na timu hiyo.
MUNICH, UJERUMANI: STAA wa Chelsea, Nicolas Jackson alifanya jitihada zisizo za kawaida kuhakikisha ndoto yake ya kujiunga na Bayern Munich inatimia.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka Ujerumani, Jackson alikataa sehemu ya pesa aliyopewa na Bayern kama bonasi ya usajili ili kuhakikisha anajiunga na timu hiyo.
Mshambuliaji huyo wa Chelsea alikamilisha uhamisho wa mkopo wa msimu mzima wenye kipengele cha kumnunua jumla siku ya mwisho ya dirisha la usajili.
Bayern inaweza kumnunua Jackson kwa ada ya Pauni 56 milioni ikiwa itaridhishwa na kiwango chake.
Hata hivyo, uhamisho huo ulikaribia kufeli baada ya Chelsea kuiambia Bayern imesitisha kumtoa staa huyo kwa mkopo baada ya kuumia kwa Liam Delap katika mchezo dhidi ya Fulham.
Wakati Chelsea inaipa Bayern taarifa hiyo, Jackson na wawakilishi wake tayari walishawasili Ujerumani na licha ya kuambiwa hivyo, yeye na wakala wake walisisitiza hawatorudi nyuma.
Baada ya kugoma na kusisitiza hawezi kurudi Chelsea, mazungumzo yaliendelea tena saa chache kabla ya kufungwa kwa dirisha, lakini Chelsea iliongeza ada ya mkopo kutoka Pauni 13 milioni hadi Pauni 14.3 milion, jambo ambalo liliweka dili hilo matatani kwa sababu Bayern haikuwa tayari kulipa kiasi hicho.
Lakini wakati Bayern imekata tamaa na kusema haiwezi kulipa kiasi hicho, Nyota huyo wa Senegal mwenye umri wa miaka 23, pamoja na wakala wake inadaiwa walikubali kutochukua kiasi chochote katika dili hilo ili kusaidia Bayern kufidia ongezeko la ada.
Katika dirisha lililopita, pia wakala wa Benjamin Sesko alikubali kupoteza sehemu ya kamisheni yake ili kumsaidia nyota huyo wa kimataifa wa Slovenia kujiunga na Manchester United.
Jackson, ambaye alisajiliwa na Chelsea akitokea Villarreal mwaka 2023, anatarajia kucheza mechi yake ya kwanza Septemba 13 dhidi ya Hamburg.