Sikia hii ya Mario Balotelli, nusura afe

PARIS, UFARANSA. STRAIKA, Mario Balotelli nusura apoteze maisha baada ya kupaliwa na pilipili aliyobugia kwa wingi akidhani kuwa ni tomato sosi katika mlo wake wake alipokuwa Marseille ya Ufaransa.

Fowadi huyo wa zamani wa Manchester City na Liverpool amekuwa mwingi wa vituko kwenye maisha yake, lakini hii ilikuwa mbaya kwa sababu pilipili ilikuwa kali na nusura ihatarishe maisha yake.

Na hilo liliwekwa wazi na mchezaji mwenzake wa zamani, Florian Thauvin, ambaye walikuwa pamoja Marseille, aliyesema Balotelli alibugia pilipili nyingi ya harissa akidhani kuwa ni tomato.

Winga, Thauvin, ambaye aliwahi kuichezea pia Newcastle, alikutana na Balotelli huko Marseille mwaka 2019.

Thauvin, 31, alisema: “Mario Balotelli alisajiliwa Marseille. Tulikuwa kwenye kambi ya kujiandaa na mechi, ulikuwa muda wa kula. Kipindi hicho, Adil Rami naye alikuwapo na yeye siku zote mlo wake ulikuwa lazima uwe na pilipili ya harissa mezani. Hivyo, mpishi alihakikisha kibakuli cha harissa hakikosekani mezani kwa ajili ya Adil. Balotelli alikuja, hakujua hilo.

“Hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kwenye kambi ya kujiandaa na mechi, hivyo kila kitu kilikuwa kipya kwake. Alijipakulia mwenyewe tambi, kisha akaenda kwenye kibakuli cha harissa akidhani ni tomato sosi. Akaanza kumimina kwenye tambi zake, kisha akachukua pande kubwa akabugia.

“Sisi tulibaki kutazamana usoni. Tulidhani anajua anachokifanya. Tulikuwa hatumfahamu, ilikuwa mbaya sana.”