Shearer amwangushia jumba bovu Sesko
Muktasari:
- Straika huyo wa Slovenia amekuwa na mwanzo mgumu katika maisha yake huko England, akiwa amefunga mabao mawili tu katika mechi 12 alizochezea timu yake mpya.
NEWCASTLE, ENGLAND: GWIJI wa Newcastle United, Alan Shearer amembebesha lawama straika Benjamin Sesko kuwa ndiye chanzo cha mambo magumu kwenye kikosi cha Manchester United msimu huu.
Straika huyo wa Slovenia amekuwa na mwanzo mgumu katika maisha yake huko England, akiwa amefunga mabao mawili tu katika mechi 12 alizochezea timu yake mpya.
Ubutu wa Sesko mbele ya magoli ya wapinzani bila ya shaka yameathiri kwa kiwango kikubwa mipango ya Man United chini ya kocha wao Ruben Amorim.
“Sesko ametaabika tena. Amefunga mara mbili tu katika mechi zake 12 na aliingizwa kwenye mechi ya mwisho zikiwa zimebaki dakika 30 na alikuwa na nafasi mbili za wazi kabisa za kufunga,” amesema Shearer.
“Walimtengenezea nafasi za kutosha. Anapaswa kufanya vizuri na kuwa mwepesi kwenye mpira. Hawezi kuwa na muda wa kutosha kwenye Ligi Kuu England, anapaswa kufanya haraka kwenye matumizi yake ya mguu wa kulia.
“Ile nafasi ya kwanza ilikuwa ya wazi kabisa, najua amepoteza hali ya kujiamini, lakini kama mshambuliaji wa kati, unapopata nafasi kama ile hupaswi kumruhusu beki wa kati anakuja kukudhibiti kama alivyofanya Van de Ven.
“Najua anapambana na hali ya kujiamini, lakini anapaswa kufanya vizuri. Hakuna aliyependa kuona anatoka nje kwa maana ameumia, wakati goti lake lilionekana kuwa sawa kabisa. Anapaswa kupambana.”