Sikia! Al Nassr yaendelea kukomaa dili la Casemiro
Muktasari:
- Casemiro alijiunga na Man United mwaka 2022 akitokea Real Madrid kwa ada ya Pauni 60 milioni amekuwa mhimili mkubwa kwenye safu ya kiungo.
KLABU ya Al Nassr ya Saudi Arabia inataka kumsajili kiungo wa kati wa Manchester United, Casemiro, ambaye mkataba wake na Mashetani Wekundu unamalizika mwishoni mwa msimu huu.
Casemiro alijiunga na Man United mwaka 2022 akitokea Real Madrid kwa ada ya Pauni 60 milioni amekuwa mhimili mkubwa kwenye safu ya kiungo.
Al-Nassr tayari ina mastaa wakubwa akiwamo Cristiano Ronaldo, Sadio Mane na Marcelo Brozovic na imekuwa ikimwinda Casemiro kwa muda mrefu.
Waarabu hao wanajaribu kumtumia staa wake, Ronaldo kama sehemu ya ushawishi ili kumpata Casemiro kwa sababu aliwahi kucheza naye kikosini Madrid.
Awali, Casemiro alionekana kuwa asingeendelea kuwepo Man United kwa msimu huu lakini kiwango chake alichoonyesha katika dakika za mwisho kilisababisha mabosi wazuie mpango wa fundi huyo kuuzwa.
Dusan Vlahovic
MANCHESTER United ipo kwenye kinyang’anyiro cha kuvaana na Atletico Madrid na Barcelona kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa Juventus na timu ya taifa ya Serbia, Dusan Vlahovic, ambaye mkataba wake na Juventus unafika tamati mwisho wa msimu ujao.
Vlahovic alisajiliwa na Juve Januari 2022 kutoka Fiorentina kwa ada ya takribani Euro 80 milioni, na mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwakani.
Micky van de Ven
REAL Madrid imeonyesha nia ya kumsajili beki wa kati wa Tottenham Hotspur, Micky van de Ven, ambaye thamani yake inakadiriwa kufikia Pauni 70 milioni.
Van de Ven alijiunga na Spurs mwaka 2023 kutoka Wolfsburg kwa ada ya takribani Euro 43 milioni, na tangu wakati huo amecheza mechi za michuano yote.
Mchezaji mwenyewe yupo tayari kuondoka na amevutiwa sana na ofa ya Madrid.
Lionel Messi
KLABU ya Inter Miami kutoka Marekani iko mbioni kumsainisha mkataba mpya wa muda mrefu staa wake Lionel Messi, 38, ambaye mkataba wake wa sasa unamalizika mwisho wa mwaka huu. Messi ambaye ameisaidia Miami kutwaa Leagues Cup mwaka 2023, huku akifunga mabao 25 katika msimu huo. Amekubali kusaini mkataba huo mpya ambao utakuwa na ongezeko la mshahara tofauti na ule wa sasa.
Federico Chiesa
WINGA wa Liverpool na timu ya taifa ya Italia, Federico Chiesa, 27, anaweza kuondoka katika timu hiyo kwenye dirisha dogo la Januari na kurejea Serie A.
Chiesa anahusishwa kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Liverpool na katika dirisha lililopita pia aliomba kutolewa hata kwa mkopo lakini ilishindikana.
Joshua Zirkzee
MANCHESTER United ipo tayari kumruhusu mshambuliaji wake wa kimataifa wa Uholanzi, Joshua Zirkzee, 24, kuondoka katika dirisha lijalo la majira ya baridi baada ya kuipata saini ya mshambuliaji wa kimataifa wa Slovenia, Benjamin Sesko, 22. Zirkzee sio miongoni mwa washambuliaji wanaopewa nafasi kubwa ya kucheza chini ya kocha Ruben Amorim na msimu huu amecheza mechi tatu za michuano yote.
Conor Gallagher
TOTTENHAM ni kati ya klabu kadhaa zinazotaka kumsajili kiungo wa kati wa Atletico Madrid na timu ya taifa ya England, Conor Gallagher, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Mabosi wa Spurs walionyesha nia ya kumsajili Gallagher tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi lakini changamoto ilikuwa ni kiasi kikubwa cha pesa kilichohitajika na Atleti.
Thomas Kristensen
AC Milan inataka kuipiku Aston Villa katika harakati za kumsajili beki wa kati wa Udinese na timu ya taifa ya Denmark, Thomas Kristensen, katika dirisha lijalo la majira ya baridi. Villa ilijaribu kumsajili katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu lakini dili halikufanikiwa. Kristensen ni beki mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi, jambo linalomfanya kuwa chaguo linalofaa kikosini.