Shabiki England aweka nyumba rehani
Muktasari:
- Milne, mwenye umri wa miaka 62, alijizolea umaarufu mkubwa wakati wa Kombe la Dunia la FIFA mwaka 2022 lililofanyika nchini Qatar, baada ya picha zake kusambaa mitandaoni.
LONDON, ENGLAND: SHABIKI lialia wa timu ya taifa ya England, Andy Milne, amefichua kuwa yuko katika mchakato wa kuuza nyumba ili kupata pesa za kufanikisha safari ya kwenda kutazama mashindano ya Kombe la Dunia litakalopigwa huko Marekani, Mexico na Canada mwaka huu.
Milne, mwenye umri wa miaka 62, alijizolea umaarufu mkubwa wakati wa Kombe la Dunia la FIFA mwaka 2022 lililofanyika nchini Qatar, baada ya picha zake kusambaa mitandaoni.
Mwaka huu, amepanga kwenda Marekani ambako mechi za England zitachezwa na anataka kuhudhuria kila mchezo wa taifa hilo. Hata hivyo, mpango wake wa kukaa Marekani kwa wiki saba utahitaji gharama kubwa kutokana na kupanda kwa bei ya tiketi na malazi.
Kombe la Dunia la mwaka huu linatajwa kuwa ghali zaidi katika historia, na mashabiki wameshaanza kulalamika kuwa gharama ni kubwa sana. Inakadiriwa kuwa mashabiki kutoka England tu watatakiwa kutumia zaidi ya Dola 10,000 kuifuatilia timu yao hadi fainali. Kwa mechi za makundi pekee dhidi ya Croatia, Ghana na Panama, mashabiki wanapaswa kulipa walau Pauni 526.
Kutokana na gharama hizo, Milne ameamua kuchukua hatua kubwa ya kuweka sokoni nyumba yake iliyopo Northwich, Cheshire, ambayo anaiuza kwa Pauni 350,000 ili kusaidia kugharamia safari yake. Kwa kawaida alikuwa akiikodisha nyumba hiyo, lakini amesema umefika wakati wa “kuchukua faida” baada ya kuimiliki kwa miaka 27. Akizungumza na Daily Mirror, amesema: “Naiuza ili niende Kombe la Dunia. Mashindano ya Qatar yalikuwa zawadi yangu binafsi baada ya kuweka akiba kwa miaka mingi. Nimekuwa na nyumba mbili kwa miaka 27, hivyo nimeona huu ni wakati sahihi wa kuuza.”
“Nataka kuhudhuria mashindano hadi mwisho. Nitaenda Marekani Juni 3 na nitakaa huko kwa wiki saba, hivyo itagharimu fedha nyingi.”
Milne pia alieleza kuwa atajaribu kupunguza gharama kadri iwezekanavyo, ikiwa ni pamoja na kulala kwa marafiki (couch surfing) katika miji mbalimbali kama Mexico, Dallas na Vancouver.
Aliongeza kuwa gharama za usafiri ni kubwa, hivyo alinunua tiketi za ndege mapema ili kupata nafuu.
Milne aliwahi kuwa gumzo mtandaoni baada ya picha yake kusambaa akiwa ameshika nakala ya kombe la Dunia, huku baadhi ya mashabiki wakisema anafanana na kocha wa zamani wa England, Steve McClaren.