Senegal yabeba ubingwa Afcon 2025
Muktasari:
- Kiungo wa Villarreal Pape Gueye alifunga bao pekee katika dakika ya nne ya muda wa ziada na kuifanya Senegal kushinda 1-0 na hivyo kunyakua taji la Afcon kwa mara ya pili ndani ya miaka minne.
RABAT, MOROCCO: Senegal imeichapa Morocco na kushinda Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya pili, lakini baada ya fainali hiyo kuchafuliwa na tukio la kuondoka kwa wachezaji wa Simba wa Teranga uwanjani wakati wenyeji walipopewa penalti ya dakika za majeruhi.
Kiungo wa Villarreal Pape Gueye alifunga bao pekee katika dakika ya nne ya muda wa ziada na kuifanya Senegal kushinda 1-0 na hivyo kunyakua taji la Afcon kwa mara ya pili ndani ya miaka minne.
Mchezo huo ulichafuliwa na utata baada ya kocha wa Senegal, Pape Thiaw kujaribu kuiongoza timu yake kuondoka uwanjani wakati Morocco ilipopewa penalti katika dakika ya 98 wakati beki El Hadji Malick Diouf alipomuangusha Brahim Diaz ndani ya boksi.
Wakati wachezaji walirejea uwanjani baada ya dakika 16, mshambuliaji wa Real Madrid, Diaz alikwenda kupiga penalti, lakini alishindwa kuifunga baada ya Edouard Mendy kudaka mkwaju huo.
Thiaw, 44, alikasirishwa na refa, Jean Jacques Ndala, ambaye alitoa penalti baada ya kuangalia tukio hilo kwenye VAR kwa kufuta bao la upande wake dakika chache zilizopita na nakutaka kwenda kujiridhisha kwenye VAR.
Mshambuliaji wa Crystal Palace, Ismaila Sarr alifunga, lakini bao lake lilifutwa kwa madai kwamba Abdoulaye Seck alimwangusha Achraf Hakimi.
Golikipa wa Senegal, Mendy alielekea chumbani, lakini alirejea uwanjani baada ya Sadio Mane kuwashawishi wachezaji wenzake kumaliza mchezo.
Gueye alifunga bao la pekee la mchezo kwa mchezo wa kuvutia katika dakika ya 94. Diaz, kwa upande mwingine, alitolewa katika muda wa ziada wakati Morocco ilipokosa nafasi ya kushinda taji lao la kwanza la Afcon tangu 1976.
Hali si nzuri kwa soka la Afrika
Mshambuliaji wa zamani wa Wimbledon, Efan Ekoku alimkosoa Thiaw na wachezaji wake, akisema kuondoka kwao uwanjani "si kitu kizuri kwa soka la Afrika".
"Ilikuwa laini," Ekoku alisema. "Ilikuwa ujinga na ni kosa la El Hadji Malick Diouf, lakini uamuzi umefanywa na wachezaji wanapaswa kulifuata. "Huwezi kufanya hivyo (kuondoka uwanjani). Hata kama unahisi umedhulumiwa, unapaswa kumruhusu refa na sheria zifanye kazi. Nina huruma, lakini hii si nzuri."
Mshindi wa Afcon 2013, John Obi Mikel alisema anaelewa hasira, lakini kuondoka uwanjani "si kitu ninachotaka kuona".