Semenyo apiga goti kubeba kimwana
Muktasari:
- Kiwango chake bora ndani ya uwanja kimefanya timu nyingi kumsaka hasa baada ya kufahamika bei yake anayouzwa kuwa ni Pauni 75 milioni kwa mujibu wa klabu yake ya Bournemouth.
LONDON, ENGLAND: MSHAMBULIAJI Antoine Semenyo amekuwa akisakwa kwelikweli kuelekea dirisha lijalo la usajili kutokana na kile anachofanya huko Bournemouth, lakini kwa wanaomtaka nje ya uwanja hilo amelifunga rasmi baada ya kumchumbia mrembo Jordeen Buckley.
Staa huyo amefunga mabao 11 na kuasisti mara tatu katika mechi 12 msimu huu.
Kiwango chake bora ndani ya uwanja kimefanya timu nyingi kumsaka hasa baada ya kufahamika bei yake anayouzwa kuwa ni Pauni 75 milioni kwa mujibu wa klabu yake ya Bournemouth.
Huko kwenye soka, Semenyo bado yupo sokoni, lakini nje ya uwanja, soko lake limefungwa. Staa huyo kipenzi cha mashabiki wa Bournemouth alipiga goti kuomba kumchumbia Jordeen na kuposti picha zake kwenye mitandao ya kijamii.
Sambamba na picha nane zilizokuwa zikiwaonyesha wawili hao kwenye furaha kubwa, mrembo Jordeen aliandika kwenye Instagram: “Daima nitakuwa kwenye hii pete nzuri. Wimbo wa Solomon 3:4, nimempata anayependezwa na moyo wangu.’€
Semenyo aliandaa tukio hilo la mahaba kwa ustadi mkubwa baada ya kuruhusiwa kuondoka kwenye kambi ya timu ya taifa ya Ghana kutokana na kupata maumivu ya enka ambayo yalimfanya akose mechi ya kirafiki dhidi ya Korea Kusini. Bournemouth ilikuwa akaunti ya kwanza kutuma ujumbe wa pongezi kwa wapendanao hao.