Sehemu Tano atakazotua Ronaldo

Friday May 14 2021
ronaldo pic

MAISHA ya Cristiano Ronaldo huko Juventus yanaonekana kuzidi ugumu siku hadi siku na kuna uwezekano mkubwa akaondoka kwenye viunga hivyo katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

Ronaldo anatajwa kuondoka kwa sababu ya muenendo mbaya wa Juventus kwa msimu huu ambapo imeshindwa hata kutetea taji lao la Ligi Kuu Italia.

Mbali ya kutetea taji Juve imetolewa kwenye hatua ya 16 bora ya michuano ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya FC Porto.

Cristiano alisajiliwa kwa mkataba wa bei bei mbaya na Juventus kwa matumaini kwamba uwepo wake ungewasaidia kutwaa taji wanalilohitaji sana la Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini mambo yamekuwa magumu.

Matukio haya yametoa ishara ya fundi huyu kuwa kwenye mstari mwekundu wa kuhitaji kuondoka kwenye viunga hivyo mwisho wa msimu na hizi hapa ni timu tano anazotarajiwa kujiunga nazo mwisho wa msimu.


Advertisement

Sporting Lisbon

Kuna uwezekano pia akarudi kwenye timu yake ya utotoni Sporting Lisbon ambayo mara kadhaa magazeti kutoka Ureno yamekuwa yakiripoti tetesi zake za kurejea.

Hata hivyo, dili la kutua kwenye viunga hivi halipewi asilimia nyingi kwa sababu ya bei yake kwenye dirisha lijalo.

Mpunga ambao Juventus inauhitaji ili kumuuza fundi huyu unatajwa kuwa mkubwa ambao inaweza kuwa shida kwa Lisbon. Vilevile atalazimika kukubali kupunguziwa mshahara ili kujiunga nao ikiwa yeye ndio atalazimisha kutimka.

Real Madrid

Real Madrid imekuwa ikihaha sana tangu Ronaldo aondoke kwenye viunga hivyo na shida kubwa imekuwa kwenye eneo lao la ushambuliaji.

Uwepo wa Eden Hazard kwenye kikosi chao hauonekani kuwa na msaada wowote kwani anaandamwa na majeraha ya mara kwa mara tangu atue akitokea Chelsea na yeye ndio alitegemewa kwenda kuziba pengo la Ronaldo.

Wababe hao vilevile wamekuwa kwenye nyakati ngumu kwa sababu hawana uhakika wa kuchukua ubingwa na msimu huu wameishia nusu fainali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa.


Man United

Urejeo wake ndani ya Old Trafford unaweza kuwa faida kubwa kwa Man United na EPL kwa ujumla kwenye mlengo wa kibiashara.

Man United inahusishwa kuwa na nafasi kubwa ya kuipata huduma yake kutokana na muenendo mzuri iliokuwa nao ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Man City na kuingia fainali ya Europa League.

Sababu hizi zinatajwa huenda zikamshawishi sana Ronaldo akaamua kujiunga nao mwisho wa msimu.

Vilevile Jorge Mendes amekuwa na uhusiano mzuri na baadhi ya mabosi wa Man United jambo linalozidisha uwezekano wa dili hilo kukamilika.


Inter Miami

Inter Miami ya Marekani pia ina nafasi ya kumsajili kutokana na uwezo wao wa kipesa na ushawishi wa mmiliki wao David Beckam ambaye inaamika ana uhusiano mzuri na Ronaldo.

Lakini bado kuna timu nyingine nyingi kutoka za ligi hiyo ya Marekani zitakazohitaji saini yake katika dirisha hilo. Hivyo Miami itakumbana na upinzani.


Juventus

Mbali ya tetesi mbali mbali zinazomhusisha na kuondoka, bado kuendelea kusalia kwenye viunga vya Juventus kunapewa nafasi kubwa kwa sababu bado ana mkataba na wababe hao hadi dirisha la majira ya kiangazi la msimu ujao.

Kitendo cha kukosa taji la Serie A kwa msimu huu ni anguko kubwa kwa Juventus, hivyo katika msimu ujao itahitaji kujenga kikosi chao na kulitwaa taji hilo kutoka kwa Inter Milan.

Lakini ikiwa Ronaldo mwenyewe atahitaji kuondoka, Juve haitakuwa na chaguo ila kumuuza.

Advertisement