Scott Carson astaafu vizuri Man City
Muktasari:
- Carson aliitumikia Man City kwa miaka minne baada ya kujiunga jumla akitokea Derby County mwaka 2021. Kipa huyo alianza kuitumikia miamba hiyo ya Etihad kwa mkopo wa misimu miwili.
MANCHESTER, ENGLAND: ALIYEKUWA kipa wa Manchester City, Scott Carson ametangaza kustaafu soka la kulipwa.
Carson, 40, aliposti kwenye mtandao wa kijamii kubainisha uamuzi wake huo, alipoandika: “Baada ya safari ndefu ya kukaa kwenye ile milingoti, umefika wakati wa kuziweka pembeni glovu zangu za kudakia. Soka limenipa kila kitu, kumbukumbu, marafiki na nyakati bora kabisa sizizosahaulika. Shukrani kwa kila mchezaji mwenzangu, kocha, mashabiki na klabu. Ni heshima kubwa kuwa kwenye hii timu.”
Carson aliitumikia Man City kwa miaka minne baada ya kujiunga jumla akitokea Derby County mwaka 2021. Kipa huyo alianza kuitumikia miamba hiyo ya Etihad kwa mkopo wa misimu miwili.
Alicheza mechi mbili tu za Ligi Kuu England, hiyo ikiwa na maana aliigharimu Man City Pauni 4 milioni kwa kila mechi. Mechi yake ya kwanza Man City katika ligi alicheza dhidi ya Newcastle United mwaka 2021, wakati mechi yake ya pili alicheza kwa dakika 17 dhidi ya Sporting Lisbon kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka uliofuatia.
Carson amevuna Pauni 8.5 milioni kwa miaka yake sita Man City, hiyo ikiwa ni wastani wa Pauni 2.8 milioni kwa kila sevu aliyofanya na wastani wa Pauni 354,000 kwa kila mguso wa mpira.
Amenyakua mataji tisa, ikiwamo manne ya Ligi Kuu England na taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wachezaji wenzake wa zamani kipa huyo walitumia nafasi yao kumpongeza Carson na Erling Haaland amesema: “Nitakumis rafiki, kila la heri,” wakati Ilkay Gundogan alikomenti kwa kuandika: “Gwiji! Ilikuwa ni furaha kubwa.”
Kalvin Phillips aliandika: “Gwiji Scotty ilikuwa furaha.” Na Nathan Ake amesema: “Hongera kwa maisha yako rafiki!!”
Kipa wa zamani wa Manchester United, Ben Foster naye amesema: “Kiwango bora kabisa Scotty.”
Katika maisha yake ya ukipa, Carson aliichezea mechi tisa Liverpool, lakini pia alipita kwenye klabu za Aston Villa, West Brom, Wigan, Charlton, Sheffield Wednesday na Leeds United.