De Bruyne ampigia debe Grealish Napoli

Muktasari:
- Grealish ameonyeshwa mlango wa kutokea na Manchester City na hajajumuishwa kabisa hata katika kikosi kinachoshiriki Kombe la Dunia kwa sasa.
NAPLES, ITALIA: KIUNGO wa Manchester City Kevin de Bruyne ambaye anatarajiwa kujiunga na Napoli katika dirisha hili inadaiwa kumuomba kocha wa Napoli, Antonio Conte amsajili Jack Grealish.
Grealish ameonyeshwa mlango wa kutokea na Manchester City na hajajumuishwa kabisa hata katika kikosi kinachoshiriki Kombe la Dunia kwa sasa.
De Bruyne ambaye ameshafanya makubaliano na Napoli na anatarajiwa kujiunga nao baada ya kumalizika kwa mkataba wake na Man City mwisho wa mwezi huu ana matumaini Conte atatimiza ombi lake la kumsajili fundi huyo.
Man City iko tayari kupoteza fedha nyingi kwa kumuuza kwa bei ya hasara Grealish ambaye ilimnunua kwa Pauni 100 milioni kutoka Aston Villa miaka minne iliyopita.
Hata hivyo, ili Grealish mwenye umri wa miaka 29, ajiunge na Napoli atatakiwa kukubali kupunguza mshahara wake anaupokea kwa sasa wa Pauni 300,000 kwa wiki na inaelezwa yeye mwenyewe yupo tayari kwa hilo kwani anataka sana kupata nafasi ya kucheza ili ajumuishwe tena katika kikosi cha timu ya taifa ya England kwa ajili ya Kombe la Dunia mwakani.
Mbali ya Napoli, Everton pia inatajwa inahitaji kumsajili staa huyu lakini yeye mwenyewe anaonekana kutamani zaidi kwenda Italia.
Tovuti ya The Sun, Jumatatu ya wiki iliyopita iliripoti Napoli ina bajeti ya Pauni 45 milioni kwa ajili ya kumsajili Grealish pia ikishindikana itatua kwa Alejandro Garnacho wa Manchester United, lakini inataka mmoja tu kati yao.
Mabingwa hao wa Serie A chini ya Conte wanaweza kuanza kampeni yao ya kutetea ubingwa wakiwa na wachezaji sita wa zamani wa Ligi Kuu England kwenye kikosi chao ikiwa watafanikisha usajili wa Grealish.
Hadi sasa katika kikosi chao ina Scott McTominay, Billy Gilmour, Romelu Lukaku na Philip Billing, pia De Bruyne ambaye bado hajatangazwa.