Saudi arabia yaisapraizi Uruguay
Muktasari:
- Matokeo hayo yameifanya Saudi Arabia kuendelea kuaminiwa kama moja ya timu zinazoweza kufanya maajabu katika michuano hiyo huku Uruguay, ambayo ilionekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda kutokana na uzoefu wake, ikishindwa kutumia ubora wake kupata pointi tatu muhimu.
MIAMI, MAREKANI :SAUDI Arabia imeanza fainali yake ya Kombe la Dunia 2026 kwa matokeo ya kuvutia baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Uruguay katika mchezo wa Kundi H uliopigwa mjini Miami usiku wa kuamkia leo, Jumanne.
Matokeo hayo yameifanya Saudi Arabia kuendelea kuaminiwa kama moja ya timu zinazoweza kufanya maajabu katika michuano hiyo huku Uruguay, ambayo ilionekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda kutokana na uzoefu wake, ikishindwa kutumia ubora wake kupata pointi tatu muhimu.
Uruguay ilianza mechi kwa kasi na kutengeneza nafasi ya kwanza mapema kupitia Maximiliano Araujo lakini kipa wa Saudi Arabia, Mohammed Al-Owais, alifanya kazi kubwa kuokoa shuti hilo.
Saudi Arabia nayo ilijibu mashambulizi kupitia nahodha wake Salem Al-Dawsari ambaye alijaribu bahati yake kwa shuti la mbali lakini mpira huo ulipaa nje kidogo ya lango.
Kadri dakika zilivyosonga, Uruguay iliendelea kutawala umiliki wa mpira huku Federico Vinas akimlazimisha Al-Owais kufanya tena kazi ya ziada baada ya kuokoa nafasi kwa kichwa.
Hata hivyo, Saudi Arabia ndiyo iliyokuwa ya kwanza kushangilia baada ya kufunga bao dakika ya 41 kupitia beki Abdulelah Al-Amri.
Bao hilo lilitokana na mpira wa kona uliopigwa na Musab Al-Juwayr ambapo kichwa cha Mohamed Kanno kiliokolewa na kipa mkongwe Fernando Muslera kabla ya Al-Amri kuutumbukiza wavuni.
Kwa Saudi Arabia, bao hilo lilikuwa la kihistoria kwani lilivunja rekodi ya michezo 16 ya Kombe la Dunia bila kufunga bao la kwanza tangu walipoifunga Ubelgiji mwaka 1994.
Kocha wa Uruguay, Marcelo Bielsa, alifanya mabadiliko mawili kipindi cha mapumziko jambo lililoibadilisha kabisa sura ya mchezo.
Uruguay ilianza kushambulia kwa nguvu zaidi huku Al-Owais akiendelea kuwa kikwazo kikubwa mbele ya washambuliaji wa La Celeste.
Vinas alikosa nafasi nyingine nzuri ya kusawazisha kabla ya Manuel Ugarte kugonga mwamba kwa shuti kali la mbali lililowaacha mashabiki wa Saudi wakishika mioyo.
Nyota wa Real Madrid, Federico Valverde, naye alianza kuonyesha kiwango chake baada ya mabadiliko ya kimfumo ya Bielsa, lakini mashuti yake yalishindwa kuzaa matunda.
Presha ya Uruguay hatimaye ilizaa matunda dakika ya 80 pale Maximiliano Araujo alipofunga bao la kusawazisha baada ya Al-Owais kuokoa tena kichwa cha Vinas lakini mpira ukamkuta Araujo aliyemalizia kwa utulivu.
Baada ya bao hilo Uruguay iliongeza kasi kutafuta ushindi huku Brian Rodriguez akikaribia kufunga bao la pili kwa shuti kali lililopita karibu na lango.
Sare hiyo ina maana kuwa timu zote nne za Kundi H zina pointi moja baada ya raundi ya kwanza kufuatia Hispania kushikwa na Cape Verde katika mchezo mwingine wa kundi hilo.
Saudi Arabia sasa itaelekeza nguvu zake katika mchezo mgumu dhidi ya mabingwa wa dunia wa mwaka 2010, Hispania, huku Uruguay ikitarajia kurejea kwenye mstari wa ushindi itakapocheza dhidi ya Cape Verde.