Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siku 17 za heshima, rekodi Msimbazi


WEKUNDU wa Msimbazi, Simba wamebakiza mechi sita ndani ya siku 17 ili kujiondoa katika kivuli cha watani wao wa jadi, Yanga katika kumaliza ukame wa mataji ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB uliodumu misimu minne mfululizo.


Kwa sasa Simba ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 61, pointi mbili nyuma ya vinara Yanga 63. Tofauti hiyo ndogo imeifanya kila mechi iliyobaki kuwa sawa na fainali kwa timu zote mbili huku makosa machache yakiwa na uwezo wa kubadilisha uelekeo wa mbio za ubingwa.

Kinachofanya vita hii kuwa ya mvuto ni timu zote mbili hazina ratiba ya mechi za ligi pekee. Kati ya Juni 17 na Juni 30, zitacheza mechi tano kila moja zikiwemo nne za ligi na moja ya Kombe la Shirikisho la CRDB zikisaka tiketi ya fainali ya michuano hiyo jambo linaloongeza presha.

Ndani ya siku hizo 17, kuna wastani wa mechi moja kuchezwa ndani ya siku tatu kuanzia Juni 17 hadi Julai 4 na kuna mechi tatu za nje ya Dar es Salaam.

Simba itaanza safari hiyo ugenini dhidi ya Mbeya City, Juni 17, kabla ya kukutana na Coastal Union pale Arusha kwenye nusu fainali ya Kombe la CRDB Juni 20 Uwanja wa Kumbukumbu wa Sheikh Amri Abeid.

Juni 24, itakuwa ugenini Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar kabla ya kumalizia mechi mbili za mwisho kwenye ligi Dar es Salaam dhidi ya Singida Black Stars na KMC, Juni 27 na 30. Kisha matokeo dhidi ya Coastal yataamua Simba icheze fainali ya CRDB Julai 4.

Kwa upande wa Yanga, kazi inaanza Juni 18 ugenini dhidi ya Fountain Gate jijini Arusha, kabla ya kuvaana na Azam kwenye nusu fainali ya Kombe la CRDB Juni 21 jijini Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Ratiba yao inakuwa ngumu zaidi kwani baada ya hapo wanakutana tena na Azam kwenye ligi Juni 24, mechi ikipelekwa New Amaan Complex, Zanziabr, kabla ya kucheza na TRA United Juni 27 na JKT Tanzania Juni 30, zote ikiwa Dar es Salaam za kuhitimisha msimu wa ligi.

Simba inakutana na Mbeya City na Mtibwa Sugar ambazo zinapambana kuwa mbali na hatari ya kushuka daraja, wakati Singida Black Stars ikiwa moja ya timu ambazo zimekuwa zikiwasumbua ikihitaji kuweka hesabu sawa za kumaliza nne bora.

Kwa Yanga, mtego mkubwa zaidi unaonekana kuwa Azam. Kukutana na timu hiyo mara mbili ndani ya siku tatu kunahitaji umakini mkubwa kwani mechi ya kombe inaweza kuathiri hali ya kikosi kabla ya pambano la ligi ambalo linaweza kuwa na athari kubwa kwenye mbio za ubingwa.

Hata hivyo, hatari kubwa zaidi kwa timu zote si ubora wa wapinzani wao pekee bali idadi ya mechi ambazo zimesalia na siku ambazo mechi hizo zitatakiwa kucheza. Ndani ya siku 17, makocha watalazimika kusimamia uchovu wa wachezaji, majeraha na adhabu za kadi huku wakitafuta matokeo bora.

Iwapo Simba na Yanga zitashinda mechi zao za nusu fainali za Kombe la CRDB, maana yake zitakuwa na mchezo mwingine wa fainali katikati ya vita ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara ikienda kushuhudiwa Dabi ya Kariakoo nyingine baada ya Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara mara mbili na fainali ya Kombe la Muungano.

Katika Dabi ya Kariakoo hizo za msimu huu, Yanga ilishinda Ngao ya Jamii bao 1-0, Simba ikashinda fainali ya Kombe la Muungano 1-0. Kisha sare kunako Ligi Kuu Bara ikianza 0-0, ikamalizia 2-2.

Takwimu za miaka minne iliyopita zinaonyesha wazi ukubwa wa kazi iliyo mbele ya Simba. Katika kipindi hicho Yanga imekuwa ikitawala soka la ndani kwa kutwaa mataji ya Ligi Kuu Bara na kufanya vizuri kwenye Kombe la CRDB huku Simba ikishuhudia mara kadhaa matumaini yake yakizimwa katika hatua za mwisho za msimu.

Pamoja na presha hiyo, kocha wa Simba, Steve Barker, ameonyesha kuridhishwa na maendeleo ya kikosi chake tangu alipowasili klabuni humo Desemba 2025.

“Jambo muhimu ni kuendelea kupigania matokeo katika kila mchezo ambao upo mbele yetu, tuna mechi moja kabla ya nusu fainali ya Kombe la FA, akili na nguvu zetu tumeelekeza hapo tunatakiwa kushinda kisha ndio tuanza kufikiria nusu fainali, kila mmoja wetu anatamani kuona tukimaliza msimu na ubingwa itakuwa ni fahari kwetu pamoja na mashabiki wetu,” alisema kocha huyo.

Lakini pamoja na matumaini hayo, ukweli unabaki kuwa Simba haina nafasi ya kufanya makosa kwani sare moja au kupoteza kunaweza kuipa Yanga mwanya wa kutengeneza tofauti kubwa zaidi huku msimu ukielekea ukingoni.

Kwa Yanga tofauti ya pointi mbili sio kinga ya ubingwa, hasa ikizingatiwa kwamba wana mechi dhidi ya Azam na TRA United ambazo zinaweza kutibua mambo.