Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Iran yanusurika, New Zealand yakosa ushindi wa kwanza

Muktasari:

  • Matokeo hayo yameiacha New Zealand ikiwa na majuto baada ya kuwa mbele mara mbili, huku Iran ikikomaa na kuondoka na pointi moja  katika mbio za kusaka tiketi ya hatua ya mtoano.

LOS ANGELS, MAREKANI: NEW  Zealand imeendelea kusaka ushindi wake wa kwanza katika historia ya Kombe la Dunia baada ya kushindwa kulinda uongozi mara mbili na kulazimisha sare ya mabao 2-2 na Iran katika mchezo wa Kundi G uliochezwa alfajiri ya leo, Jumanne, Los Angeles, Marekani.

Matokeo hayo yameiacha New Zealand ikiwa na majuto baada ya kuwa mbele mara mbili, huku Iran ikikomaa na kuondoka na pointi moja  katika mbio za kusaka tiketi ya hatua ya mtoano.

Timu hiyo ya Oceania ambayo ilikuwa na nafasi ndogo zaidi kwenye michuano hii kwa mujibu wa viwango vya FIFA, iliwashangaza wengi kwa kuanza mechi hiyo kwa kishindo.

Dakika ya saba tu, New Zealand ilipata bao la kuongoza kupitia Elijah aliyemalizia mpira uliotokana na ushirikiano mzuri kati yake na nahodha Chris Wood.

Wood alidhibiti mpira mrefu kutoka nyuma kabla ya kumpasia Sarpreet Singh aliyemrudishia mpira kwa Elijah, ambaye baada ya kubadilishana pasi nyingine na mshambuliaji huyo wa Nottingham Forest aliupiga mpira wa mrefu uliomshinda kipa Alireza Beiranvand.

Bao hilo liliwapa nguvu Wazungu hao wa Pasifiki ambao walionekana kucheza kwa kujiamini dhidi ya Iran iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo.

Iran ilianza kuamka katikati ya kipindi cha kwanza kupitia mshambuliaji wake nyota Mehdi Taremi ambaye alikaribia kusawazisha baada ya kukimbia na mpira kutoka katikati ya uwanja, lakini shuti lake liligonga mwamba.

Presha ya Iran ilizaa matunda dakika ya 32 wakati Ramin Rezaeian alipofunga bao la kusawazisha baada ya mabeki wa New Zealand kushindwa kuondoa hatari ndani ya eneo lao.

Iran iliamini imepata bao lingine kabla ya mapumziko kupitia Ali Nemati lakini mwamuzi alikataa bao hilo kwa madai ya kuotea.

Kipindi cha pili kilianza kwa Iran kuonyesha nia ya kutafuta ushindi lakini kama ilivyokuwa mwanzo wa mchezo, New Zealand ndiyo iliyowashangaza wapinzani wake.

Dakika ya 54, Elijah  aliifungia New Zealand bao la pili baada ya tena kushirikiana kwa ustadi mkubwa na Wood, aliyekuwa mhimili wa mashambulizi yote hatari ya timu hiyo.

Elijah alikokota mpira kuelekea langoni mwa Iran kabla ya kutoa pasi kwa  Wood na kisha kumalizia kwa shuti lililomshinda Beiranvand.

Bao hilo lilionyesha kiwango bora cha mshambuliaji huyo wa Motherwell ambaye aligeuka kuwa tishio kubwa kwa safu ya ulinzi ya Iran katika dakika zote 90.

Hata hivyo, kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza, Iran haikukata tamaa na iliendelea kutengeneza nafasi  kutafuta bao la kusawazisha.

Dakika ya 64, Mohammad Mohebi aliwashtua mabeki wa New Zealand waliokuwa wamejisahau kwa kufunga bao la pili la Iran kwa kichwa baada ya kupokea krosi safi kutoka kwa Rezaeian.

Bao hilo lilikuwa zawadi ya juhudi za Iran ambazo zilionekana kuongezeka kila dakika ilivyopita huku New Zealand ikianza kuchoka.

Dakika zilizobaki zilikuwa na mashambulizi ya pande zote mbili lakini hakuna timu iliyopata bao la ushindi katika mechi hiyo iliyokuwa miongoni mwa michezo bora ya mwanzo wa Kombe la Dunia 2026.

Matokeo hayo yanaifanya New Zealand kuendelea kusubiri ushindi wake wa kwanza katika Kombe la Dunia baada ya sasa kucheza mechi saba bila kushinda, huku ikibaki na sare nne na kupoteza tatu.