Sasa ni Joshua vs Wilder

PAMBANO la ngumi uzito wa juu duniani (heavyweight) kati ya mabondia Waingereza, Anthony Joshua na Dillian Whyte, lililokuwa lifanyike Jumamosi wiki hii, limefutwa kutokana na Whyte kukutwa na vimelea vya dawa za kuongeza nguvu zilizofanywa na chama cha kupambana na dawa za kulevya (VADA).

Kutokana na kuwa sio mara ya kwanza kwa Whyte kukutwa na kadhia hiyo, pambano hilo limefutwa na Whyte hatopata tena nafasi ya kupigana na Joshua ‘AJ’ ambaye sasa ana nafasi ya kuchagua bondia mpya wa kupigana naye, akiwemo Deontay Wilder aliyeweka wazi anamtaka ulingoni.

Joshua ambaye bado anatamani zaidi kupigana na Mwingereza mwenzake Tyson Fury, kama ataridhia kupigana na Wilder, pambano hilo linaweza kupangwa siku chache zijazo na kitakachochelewesha ni sehemu ya litakapofanyika.

Eddie Hearn, promota wa Joshua na bosi wa kampuni ya kusimamia masumbwi, Matchroom, bado hajaweka wazi kama mteja wake atapigana na Tyson Fury au Wilder ambao ndio wapo kwenye rada za kupigana na AJ, ikitegemeana na utayari wa Fury baada ya pambano lake dhidi ya Francis Ngannou.