Sasa dili la Gyokeres lipo pazuri
Muktasari:
- Kwenye mchakato huo, Arsenal italipa Pauni 54.8 milioni za utangalizi kisha Pauni 8.6 milioni italipa baadaye kutokana na kiwango cha staa huyo ambaye atasaini dili la miaka mitano huko Emirates.
LONDON, ENGLAND: HATIMAYE, Arsenal imekubali kulipa ada ya Pauni 63.5 milioni ili kuinasa huduma ya straika wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres.
Kwenye mchakato huo, Arsenal italipa Pauni 54.8 milioni za utangalizi kisha Pauni 8.6 milioni italipa baadaye kutokana na kiwango cha staa huyo ambaye atasaini dili la miaka mitano huko Emirates.
Wakala wa Gyokeres, Hasan Cetinkaya amekubali kukosa asilimia 10 ya kamisheni yake ili kupunguza ada ambayo Arsenal itaweza kuilipa ili Sporting wapate kiwango cha pesa walichokuwa wakihitaji.
Baada ya wiki ya mazungumzo mazito na Sporting, mabosi wa Arsenal hatimaye wamefikia makubaliano ya kunasa straika huyo na muda wowote dili hilo litathibitishwa.
Gyokeres atakuwa usajili wa nne wa Arsenal kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi baada ya kuwanasa Kepa Arrizabalaga kutoka Chelsea, Christian Norgaard kutoka Brentford na Martin Zubimendi kutoka Real Sociedad.
Arsenal inayonolewa na Mikel Arteta imekubali pia kulipa Pauni 52 milioni kunasa dili la winga wa miamba ya Stamford Bridge, Noni Madueke, ambaye alijiondoa kwenye kikosi cha The Blues kabla haya ya mechi ya fainali ya Kombe la Dunia la Klabu iliyofanyika usiku wa Jumapili.
Kocha Arteta anataka kukamilisha dili la kupata Namba 9 wake kabla ya kuanza ziara ya pre-season huko Singapore na Hong Kong wikiendi hii. Arsenal ilicheza nusu ya pili ya msimu uliopita kwenye Ligi Kuu England bila ya ya kuwa na Namba 9, hivyo ilizidiwa na Liverpool kwenye mbio za ubingwa kwa tofauti ya pointi 10 na mabao 17.
Mwanzoni ilielezwa Sporting ilihitaji Pauni 60.4 milioni ya awali na Pauni 8.6 milioni italipwa kama ziada, lakini baada ya straika Gyokeres kugoma kurudi kwenye timu hiyo, akionyesha dhamira yake ya kwenda kucheza Ligi Kuu England, miamba hiyo ya Ureno imeshusha bei kidogo.
Gyokeres alifunga mabao 54 katika mechi 52 alizocheza kwenye kikosi cha Sporting msimu uliopita na kuipa timu hiyo ubingwa wa ligi na kombe la ndani.
MAVITU YA GYOKERES 2024-2025
Amecheza: Mechi 52
Amefunga: Mabao 54
Ametoa: Asisti 13
Amekuwa: Uwanja dakika 4248
Ameonyesha: Kadi za njano 6
Amebeba: Mataji 2