Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyemsajili salah ajiuzulu Liverpool

Muktasari:

  • Edwards, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Michezo wa Liverpool kabla ya kuondoka mwaka 2022, alirejea mwaka 2024 akiwa Mtendaji Mkuu wa Operesheni za Soka wa FSG. Hata hivyo, sasa amejiuzulu mwaka mmoja kabla ya mkataba wake kumalizika.

LIVERPOOL, ENGLAND: KLABU ya Liverpool imekumbwa na pigo baada ya mmoja wa watu waliohusika kwa kiasi kikubwa kujenga mafanikio ya usajili wa nyota ndani ya muongo mmoja uliopita, Michael Edwards, kuamua kuachia nafasi yake katika Fenway Sports Group (FSG).

Edwards, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Michezo wa Liverpool kabla ya kuondoka mwaka 2022, alirejea mwaka 2024 akiwa Mtendaji Mkuu wa Operesheni za Soka wa FSG. Hata hivyo, sasa amejiuzulu mwaka mmoja kabla ya mkataba wake kumalizika.

Inaelezwa kuwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 47 aliwajulisha viongozi wa FSG kuhusu uamuzi wake tangu msimu wa vuli wa mwaka jana na tayari amemaliza kipindi chake cha taarifa ya kuondoka (notice).

Kwa mujibu wa taarifa, FSG haitarajii kumteua mbadala wake, huku Rais wa FSG, Mike Gordon, akichukua tena jukumu la kusimamia shughuli za soka za kampuni hiyo.

Wakati Edwards aliporejea, alikuwa na matumaini makubwa ya kuisimamia FSG katika mpango wa kupanua mfumo wa umiliki wa klabu nyingi. Lakini miaka miwili baadaye, hakuna maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika mpango huo.

Inaaminika kuchelewa kwa mradi huo kulimkatisha tamaa Edwards. Mbali na gharama kubwa za kununua klabu mpya, FSG pia ilikuwa na wasiwasi kutokana na kanuni mpya za UEFA zinazozidi kubana mfumo wa umiliki wa klabu.

Katika kipindi chake Liverpool, Edwards alisifika kwa kutumia mfumo wa uchambuzi wa takwimu (data analytics) kusajili wachezaji walioibadili historia ya klabu.

Chini ya usimamizi wake, Liverpool iliwasajili Mohamed Salah, Andy Robertson na Sadio Mane kwa ada ambazo zilionekana kuwa nafuu, kabla ya nyota hao kuiongoza timu kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2019 na Ligi Kuu England mwaka 2020.

Hadi sasa haijafahamika hatua inayofuata kwa Edwards, ingawa wakati alipokuwa nje ya Liverpool aliwahi kuwindwa na vigogo kama Manchester United na Chelsea.

Pamoja na kuondoka kwake, taarifa zinaeleza kuwa hakutakuwa na athari kubwa katika shughuli za kila siku za Liverpool, kwani Mkurugenzi wa Michezo, Richard Hughes, ndiye anayesimamia kwa karibu masuala ya usajili, licha ya kuripotiwa kuvutiwa na klabu kutoka Saudi Arabia.

Katika dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi, Liverpool tayari imewasajili winga Victor Munoz kutoka Osasuna na beki Jeremy Jacquet aliyewasili kutoka Rennes.

Akizungumza baada ya kuondoka kwake, Edwards alisema:

"Naondoka nikiwa naamini Liverpool ipo katika nafasi nzuri, ikiwa na watu bora, mwelekeo ulio wazi na msingi imara wa kuendelea kupata mafanikio.

"Niliporejea nilifurahishwa si tu na nafasi ya kuisaidia Liverpool katika kipindi muhimu cha mpito, bali pia kushiriki kujenga dira ya FSG katika soka kwa ujumla.

"Ingawa mradi huo mkubwa uliendelea kwa njia tofauti na tulivyotarajia mwanzoni, ninajivunia kazi kubwa ambayo timu yetu ilifanya kwa kuwasilisha kwa wamiliki mapendekezo mbalimbali yaliyofanyiwa kazi kwa kina kwa ajili ya mustakabali wa kampuni."