Ronaldo afunguka maisha magumu baada ya kustaafu soka
Muktasari:
- Ronaldo, ambaye alistaafu akiwa na miaka 34 baada ya kucheza kwa miaka 18, amesema kuacha soka kulimpa maumivu makubwa kana kwamba alikuwa amepoteza mtu wa karibu.
LOS ANGELES, MAREKANI: GWIJI wa soka wa Brazil, Ronaldo Nazario de Lima, amefunguka kuhusu kipindi kigumu alichopitia baada ya kustaafu soka mwaka 2011, akisema aliingia kwenye msongo mkubwa wa mawazo uliomfanya hata kuongezeka uzito kwa kiwango kikubwa.
Ronaldo, ambaye alistaafu akiwa na miaka 34 baada ya kucheza kwa miaka 18, amesema kuacha soka kulimpa maumivu makubwa kana kwamba alikuwa amepoteza mtu wa karibu.
"Unapoamua kuacha soka, unajisikia kama kuna mtu wa karibu amefariki dunia," alisema Ronaldo kwenye podikasti ya Futebol Legends Talks.
Mshambuliaji huyo aliyeshinda Kombe la Dunia mara mbili akiwa na Brazil (1994 na 2002), alikiri kuwa alipatwa na msongo mkubwa wa mawazo na maisha yakabadilika ghafla.
"Nilipata msongo mkubwa wa mawazo. Nilinenepa sana. Ilikuwa ngumu sana kukubali kwamba sitacheza tena."
Ronaldo alisema baadaye alijifunza kuwa maisha yanaendelea na mtu anaweza kujijenga upya, lakini alikiri ilimchukua muda mrefu kuzoea maisha bila ushindani wa uwanjani.
"Baadaye niligundua kuna mambo mengine ya kufanya maishani, lakini hamu ya kushindana ilibaki moyoni kwa muda mrefu."
Ronaldo mbali na mafanikio kwenye klabu pia alifanikiwa kutwaa makombe kadhaa akiwa na Real Madrid ambapo alicheza michezo 177 na kufunga mabao 104 akifanikiwa kutwaa makombe mawili ya La Liga, pia alizichezea Inter Milan, Barcelona, PSV na Corrinthias ambapo kwenye klabu zote alicheza michezo 518 na kufunga mabao 352.