Sancho sasa anauzwa Pauni 40 milioni tu

Muktasari:

  • Man United huko nyuma iliripotiwa kuhitaji Pauni 50 milioni kwenye mauzo ya winga huyo aliyetibuana na kocha Erik ten Hag.

MANCHESTER, ENGLAND: NDO hivyo. Manchester United sasa imefungua milango ya kumpiga bei Jadon Sancho kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi kama kutakuwa na timu itakayokuwa tayari kuweka ubaoni Pauni 40 milioni.

Man United huko nyuma iliripotiwa kuhitaji Pauni 50 milioni kwenye mauzo ya winga huyo aliyetibuana na kocha Erik ten Hag.

Na sasa ripoti zinadai, bei hiyo imeshuka na winga huyo mwenye umri wa miaka 24 atauzwa bila ya kujali ni kocha gani atakayekuwapo kwa msimu ujao kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.

Man United inalazimika kuuza mastaa wake ili kuweka sawa bili yao ili kwenda sawa na ishu ya mapato na matumizi kama ambavyo inavyohitajika kwenye Ligi Kuu England.

Sancho alikuwa na wakati mzuri kwa kipindi cha miezi sita aliyocheza kwa mkopo Borussia Dortmund na miamba huyo ya Bundesliga inapenda kubaki na huduma ya mchezaji huyo, lakini sasa watalazimika kulipa Pauni 40 milioni, ikiwa ni ada yake ya uhamisho.

Man United yenyewe ilimsajili Sancho kutoka Dortmund mwaka 2021 kwa ada ya Pauni 73 milioni na bado ana mkataba wa miaka miwili. Tangu wakati huo aliotua Old Trafford, winga huyo Mwingereza, amefunga mabao 12 na kuasisti mara sita.

Ripoti zinafichua kwamba Sancho hatakuwa na namna kama atakosa timu ya kumnunua kwenye dirisha hili, hivyo atarudi kukipiga Old Trafford, licha ya kwamba anahisi maisha yake yatakuwa magumu endapo kama kocha Ten Hag ataendelea kubaki kwenye klabu hiyo.