Sancho akubali kushusha mzigo akiitaka Juventus

Muktasari:
- Inaelezwa kwamba Juventus imekuwa ikisita kumsajili kwa sababu mbalimbali na mojawapo ni kiasi cha mshahara ambacho anakipata kwa sasa huko Old Trafford ambako alisajiliwa misimu mitatu iliyopita kwa dau la maana akitokea Borussia Dortmund.
WINGA wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Jadon Sancho mwenye miaka 25, yuko tayari kupunguza mshahara wake ili kukamilisha dili lake kutoka Manchester United kwenda Juventus, katika dirisha hili la usajili linaloendelea Ulaya.
Inaelezwa kwamba Juventus imekuwa ikisita kumsajili kwa sababu mbalimbali na mojawapo ni kiasi cha mshahara ambacho anakipata kwa sasa huko Old Trafford ambako alisajiliwa misimu mitatu iliyopita kwa dau la maana akitokea Borussia Dortmund.
Kutokana na hilo Sancho ambaye kwa wiki huwa anakunja kiasi kisichopungua Pauni 300,000 anaweza kukubali kupokea chini ya Pauni 200,000 ili kukamilisha dili ambalo huenda likamfanya aende akapate nafasi ya kucheza mara kwa mara kikosini kama ilivyo nia yake.
Hata hivyo licha ya kukubali kupunguza mshahara, Juventus bado inasuasua kwa sababu haipo tayari kutoa kiasi cha pesa kinachohitajika na Man United ambayo tayari imeshamuondoa katika mipango yake ya muda mfupi na mrefu.
Kwa sasa Manchester United inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 25 milioni kama ada ya uhamisho ya Sancho na Juventus inataka kulipa Pauni 20 milioni.
Awali Juventus ilikuwa inahitaji kukamilisha dili hili kwa kufanya mabadilishano ya wachezaji na walikuwa tayari kumruhusu kiungo Douglas Luiz kama sehemu ya ofa ili kuhakikisha kwamba wanampata mchezaji huyo. Sancho msimu uliopita alicheza Chelsea ambayo imegoma kumnunua mazima.
Rasmus Hojlund
MMSHAMBULIAJI wa Manchester United, Rasmus Hojlund 22, ni miongoni mwa wachezaji ambao Inter Milan imewaweka katika vipaumbele vyake kwa ajili ya kuwasajili katika dirisha hili la majira ya kiangazi. Hojlund ambaye msimu uliopita akiwa na Man United alicheza mechi 52 za michuano yote na kufunga mabao 52, mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2028.
Chemsdine Talbi
SUNDERLAND iko karibu kukamilisha dili la kumsajili mshambuliaji wa Club Brugge na timu ya taifa ya Morocco, Chemsdine Talbi mwenye umri wa miaka 20 ambaye msimu uliopita alicheza mechi 44 za michuano yote na kufunga mabao saba. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika ifikapo 2027 na tayari timu kibao zimwasilisha ofa zikihitaji saini yake.
Mark Travers
EVERTON inataka kumsajili kipa wa Bournemouth, Mark Travers, 26, ambaye aliivutia akiwa kwa mkopo Middlesbrough kutoka Bournemouth msimu uliopita. Travers ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2027 msimu uliopita alicheza mechi 22 za michuano yote.
Mateo Retegui
ATALANTA imekataa ofa ya Pauni 45.7 milioni kutoka Al-Qadsiah ya Saudi Arabia kwa ajili ya mshambuliaji wa kimataifa wa Italia, Mateo Retegui 26, katika dirisha hili. Inaelezwa Atalanta imekataa ofa hiyo na kusisitiza inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 51.8 milioni. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2028.
Nkunku
BBAYERN Munich imefanya mazungumzo na wakala wa Christopher Nkunku kuulizia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji huyo wa Chelsea na timu ya taifa ya Ufaransa mwenye miaka 27. Nkuku ameomba kuondoka Chelsea katika dirisha hili la usajili kwa ajili ya kujiunga na timu itakayompa nafasi kubwa zaidi ya kucheza tofauti na ilivyo sasa.
Anton Stach
LEEDS United inapamban ili kumsajili kiungo wa kati wa Hoffenheim, Anton Stach, 26, lakini inakumbana na upinzani mkali kutoka baadhi ya timu nyingine za England ambazo zinahitaji saini yake. Anton ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika itakapofika 2027, msimu uliopita alicheza mechi 39 za michuano yote.
Matt O’Riley
AS Roma inataka kumsajili kiungo wa kati wa Brighton na timu ya taifa ya Denmark, Matt O’Riley, 24, katika dirisha hili la majira ya kiangazi barani Ulaya. Benchi la ufundi la Roma limevutiwa sana na kiwango alichoonyesha supastaa huyo katika dirisha lililopita ambapo alicheza mechi 26 za michuano yote na kuonyesha kiwango bora.