Salah afunguka mazito akiichana Liverpool
Muktasari:
- Salah ameendelea kuwekwa benchi mara hii ikiwa ni katika mechi dhidi ya Leeds United ambayo ilimalizika kwa sare ya mabao 3-3, ikiwa ni mwendelezo wa mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha kwa Liverpool tangu kuanza kwa msimu huu.
LIVERPOOL, ENGLAND: MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Mohamed Salah ameishambulia timu yake na benchi la ufundi akieleza kwamba wanamtumpia lawama bila sababu kwani yeye siyo chanzo cha timu kufanya vibaya.
Salah ameendelea kuwekwa benchi mara hii ikiwa ni katika mechi dhidi ya Leeds United ambayo ilimalizika kwa sare ya mabao 3-3, ikiwa ni mwendelezo wa mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha kwa Liverpool tangu kuanza kwa msimu huu.
Mechi hiyo ilikuwa ni yatatu mfululizo kwa Salah kukaa benchi hali ambayo sasa inaonekana kumchosha.
Baada ya mchezo, Salah alisema kuna uwezekano mdogo wa kumalizia maisha ya soka katika viunga vya Liverpool, akidai kuna mtu anataka yeye ndio abebweshe lawama zote juu ya kile kinachoendelea katika timu kwa sasa.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Misri mwenye umri miaka 33, alisema: “Nimevunjika moyo sana. Nimefanya mambo mengi sana kwa ajili ya klabu hii. Kila mtu ameona hilo kwa miaka yote, hasa msimu uliopita. Inaonekana kama klabu inanigeuka. Ndivyo ninavyohisi.
Ni wazi kabisa kuna mtu anataka lawama zote ziwe juu yangu.”
Licha ya Liverpool kutwaa ubingwa msimu uliopita, msimu huu imekuwa katika hali mbaya ikishuka hadi nafasi ya nane, ikiwa pointi 10 nyuma ya vinara Arsenal.
Salah ambaye alifunga mabao 34 katika mashindano yote msimu uliopita, msimu huu ana mabao manne tu kwenye mechi 13 za Ligi Kuu England hadi sasa.
Kuhusu uhusiano wake na Slot, alisema: “Nimesema mara nyingi kuwa nilikuwa na uhusiano mzuri na kocha, lakini ghafla hatuna tena uhusiano wowote. Sijui kwa nini.
Hili halikubaliki kwangu… kama ningekuwa sehemu nyingine, klabu ingemlinda mchezaji wake.”
“Kwangu mimi, inaonekana kama wananishusha katika basi la timu kilazima kwa sababu wanaona mimi ndiye tatizo, lakini mimi sioni hivyo. Nimefanya mambo mengi kwa ajili ya klabu hii, natakiwa kupata heshima ninayostahili.”
“Nimekuwa hapa na nimefunga mabao mengi kuliko mchezaji yeyote wa kizazi hiki. Kwa kweli tangu nimeingia kwenye timu hii, sidhani kama kuna mtu amefunga mabao mengi kuliko mimi, au kutoa asisti nyingi.”
Salah alienda mbali akilinganisha kinachomtokea na kilichowahi kumkuta Harry Kane, akisema:"Nakumbuka muda fulani Harry Kane hakuwa akifunga kwa karibu mechi 10, akaja kufunga moja au mbili, lakini vyombo vya habari vilisema vikisema, ‘Ah, Harry atafunga tu’.
"Kwa Mo, wanataka niwe benchi.”
Salah ambaye hadi sasa amefunga mabao 250 akiwa na Liverpool, alisema tayari amezungumza na kocha kuhusu kuachwa benchi: “Nilikuwa na kikao na kocha. Anajua hisia zangu. Awali nilidhani ningeongeza mkataba na kumaliza maisha yangu hapa, lakini mambo hayapo kama yalivyopangwa.
"Klabu iliniahidi mengi katika dirisha la majira ya kiangazi, lakini hadi sasa nimekuwa benchi katika mechi tatu. Ninachoweza kusema ni kwamba waendelee kutimiza ahadi.”
Salah pia alimchana lejendi na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Jamie Carragher akisema: “Kwa klabu kama hii, kwa kile nilichofanya, inauma. Unatoka nyumbani kwenda katika mechi na hujui kama utaanza au la. Lakini naifahamu klabu hii vizuri. Nimekuwa hapa miaka mingi. Kesho utamuwona Carragher ananishambulia tena na tena. Sawa tu.”
Liverpool itacheza na Inter Milan katika Ligi ya Mabingwa, kesho Jumanne, kisha itarudi tena katika ligi kucheza dhidi ya Brighton Jumamosi ijayo ambayo inaweza kuwa mechi ya mwisho ya Salah kabla hajajuunga na na timu ya taifa ya Misri kuelekea AFCON nchini Morocco wiki ijayo.
“Nitakuwa Anfield, kuwaaga mashabiki, kisha nitaenda Afcon. Sijui nini kitatokea nikiwa kule.”
Kwa upande wake kocha, Slot alieleza kwa nini alimuacha Salah benchi kwenye mechi dhidi ya Leeds akisema: "Tulikuwa tunaongoza 2-0, kisha 3-2, ilikuwa muhimu zaidi kudhibiti mchezo, hatukuhitaji goli.
Kwa kawaida tukihitaji goli, kama wiki iliyopita dhidi ya Sunderland, huwa namuingiza Mo.”