Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uhondo wa masupastaa hawa kukosekana Morocco

MASTAA Pict

Muktasari:

  • Sawa, Afrika imesheheni wakali wa maana kabisa ambao wamekuwa wakionyesha viwango vikubwa kwenye ligi za huko Ulaya na kurudi Afrika kunogesha mambo katika mikikimikiki ya Afcon kama vile Victor Osimhen (Nigeria), Mohamed Salah (Misri), Brahim Díaz (Morocco) na Ademola Lookman (Nigeria) kwa kuwataja kwa uchache, hali ingekuwa tofauti kabisa kama wale wengine wenye asili ya Afrika wasingechagua kutumikia timu za taifa za Ulaya.

RABAT, MOROCCO: MASUPASTAA wengi wa soka wenye asili ya Afrika wamekuwa wakichezea mataifa ya Ulaya na kufanya mashabiki wa mchezo huo wa bara hili kukosa huduma zao matata kabisa kwenye mashindano makubwa kama ya Afcon.

Sawa, Afrika imesheheni wakali wa maana kabisa ambao wamekuwa wakionyesha viwango vikubwa kwenye ligi za huko Ulaya na kurudi Afrika kunogesha mambo katika mikikimikiki ya Afcon kama vile Victor Osimhen (Nigeria), Mohamed Salah (Misri), Brahim Díaz (Morocco) na Ademola Lookman (Nigeria) kwa kuwataja kwa uchache, hali ingekuwa tofauti kabisa kama wale wengine wenye asili ya Afrika wasingechagua kutumikia timu za taifa za Ulaya.


MASTA 01

Kylian Mbappe (Cameroon & Algeria)

Kylian Mbappe Lottin alizaliwa Desemba 20, 1998 huko Paris na kukulia Bondy, Seine-Saint-Denis, kitongoji cha kaskazini mashariki Paris.

Baba yake, Wilfrid Mbappe, ni kocha wa soka na anatokea kisiwa cha Djebale kilichopo Cameroon.

Mama yake, Fayza Lamari, ana asili ya Algeria na ni mchezaji wa zamani wa mpira wa mikono. Lakini, Mbappe amechagua kuicheza Ufaransa kwenye soka la kimataifa.


MASTA 02

Paul Pogba (Guinea)

Kiungo wa boli, Paul Pogba alizaliwa Lagny-sur-Marne, Ufaransa na wazazi wenye asili ya Guinea.

Kaka zake wawili ambao ni pacha, Florentin Pogba na Mathias Pogba, wao walizaliwa Guinea na wanachezea timu ya taifa ya soka ya Guinea.

Lakini, Pogba, ambaye kwa sasa anakipiga kwenye kikosi cha AS Monaco alichagua kuitumikia Ufaransa kwenye soka la kimataifa ambako alikiwezesha kikosi hicho cha Les Bleus kushinda Kombe la Dunia 2018.


MASTA 03

Bukayo Saka (Nigeria)

Bukayo Ayoyinka Temidayo Saka alizaliwa Septemba 5, 2001 huko Ealing, Greater London, kwa wazazi wa Kiyoruba wenye asili ya Nigeria, Adenike na Yomi Saka, akiwa ni mdogo kwenye familia ya watoto wawili.

Wazazi wake walihamia London kutoka Nigeria kama wahamiaji waliokimbia hali ngumu ya kiuchumi.

Kutokana na kuzaliwa England, Saka aliamua kuitumikia timu ya taifa ya nchi hiyo, Three Lions, huku ukweli ni kwamba staa huyo wa Arsenal alipaswa kukitumikia kikosi cha Super Eagles katika mashindano ya kimataifa.


MASTA 04

Jamal Musiala (Nigeria)

Winga machachari, Jamal Musiala alizaliwa Stuttgart, Ujerumani kwa wazazi, baba Mnigeria-Mwingereza, Daniel Richard na mama Mjerumani mwenye asili ya Poland, Carolin Musiala.

Aliishi Fulda hadi alipofikisha umri wa miaka saba kabla ya kuhamia England na familia yake na kusoma shule nchini humo kabla ya kucheza kwenye klabu za Fulham, Brentford na Wimbledon kwenye utoto wake.

Musiala angeweza kuichezea Nigeria kwenye soka la kimataifa, lakini amechagua kuitumikia Ujerumani.


MASTA 05

Memphis Depay (Ghana)

Memphis Depay alizaliwa kwenye kijiji kidogo kilichopo kusini mwa Uholanzi, Moordrecht na wazazi, ambao baba ni Mghana, Dennis Depay na mama ni Mdachi, Cora Schensema.

Haikuchukua muda mrefu kabla ya uhusiano wa wazazi wake kuvunjika na kutengana kipindi hicho Memphis alipokuwa na umri wa miaka minne.

Baba yake aliamua kuachana na familia hiyo na kuondoka zake na kumwaacha Memphis akiwa chini ya mama yake, ambaye alimfanya aitumikie Uholanzi badala ya Ghana kwenye soka la kimataifa.


MASTA 06

Romelu Lukaku (DR Congo)

Straika Romelu Lukaku alizaliwa Antwerp, Ubelgiji kwa wazazi wenye asili ya DR Congo.

Baba yake, Roger Lukaku, alikuwa mwanasoka wa kulipwa na aliitumikia timu ya taifa ya DR Congo wakati huo ilikuwa ikijulikana kama Zaire.

Kutokana na asili yake, Lukaku alipaswa kuitumikia timu ya taifa ya DR Congo kwenye mashindano ya kimataifa hususani Afcon, lakini alichagua kuitumikia Ubelgiji kwenye soka la kimataifa na kucheza timu moja na wachezaji wa maana kama Eden Hazard na Kevin De Bruyne.


MASTA 07

Serge Gnabry (Ivory Coast)

Winga Serge Gnabry alizaliwa Stuttgart, Baden-Württemberg huko Ujerumani na wazazi ambao baba ni Muivory Coast na mama ni Mjerumani.

Wakati alipokuwa mdogo, Gnabry alikuwa na kipaji kikubwa cha kukimbia riadha ya mbio fupi, lakini alichagua kujikita kwenye mchezo wa soka na kuonyesha kiwango bora kabisa tangu akiwa Arsenal na sasa Bayern Munich.

Gnabry alikuwa na uhalali wa kuichezea Ivory Coast kwenye soka la kimataifa, lakini aliichagua Ujerumani.

MASTA 08

Leroy Sane (Senegal)

Winga, Leroy Sane alizaliwa Januari 11, 1996 huko Essen na alikulia Lohrheidestadion, Wattenscheid.

Ni mtoto wa mcheza sarakasi wa zamani wa Kijerumani, ambaye alishinda medali ya shaba kwenye Olimpiki 1984, mrembo Regina Weber na baba, ambaye ni staa wa soka wa zamani wa Senegal, Souleymane Sane.

Alipewa jina la Leroy kwa ajili ya heshima ya Claude Le Roy, aliyekuwa kocha wa zamani wa baba yake. Sane angeweza kuitumikia Senegal kwenye soka la kimataifa, lakini alichagua kuitumikia Ujerumani.

Souleyman Sane, aliwahi kuwa kocha wa timu ya Taifa ya Zanzibar kuanzia mwaka 2008 hadi 2011.