Salah aendeleza makali Kombe la Dunia
Muktasari:
- Katika mechi hiyo ya kundi G, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Seattle, Washington Marekani, Misri ilikuwa ya kwanza kupata bao la dakika ya 19, lililofungwa na Emam Ashour, kisha Mohamed Hany akajifunga mwenyewe na kuisawazishia Ubeligiji dakika ya 66 na timu hizo kugawana pointi moja.
WASHINGTON, MAREKANI: LICHA ya timu ya taifa ya Misri kuanza kampeni za Kombe la Dunia kwa sare ya bao 1-1, dhidi ya Ubelgiji, ila nyota wa kikosi hicho, Mohamed Salah ameandika rekodi mbili za kibabe.
Katika mechi hiyo ya kundi G, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Seattle, Washington Marekani, Misri ilikuwa ya kwanza kupata bao la dakika ya 19, lililofungwa na Emam Ashour, kisha Mohamed Hany akajifunga mwenyewe na kuisawazishia Ubeligiji dakika ya 66 na timu hizo kugawana pointi moja.
Miongoni mwa rekodi bora iliyowekwa na Mohamed Salah ni ya kutoa asisiti ya bao la nyota wa kikosi hicho, Emam Ashour katika siku yake ya kuzaliwa ambapo leo ametimiza rasmi miaka 34.
Asisti ya bao aliyoitoa Salah leo, inamfanya kuwa mchezaji wa kwanza wa Afrika kuchangia bao katika fainali za Kombe la Dunia ikiwa ni siku yake ya kuzaliwa, kwani kabla ya hapo hakuna mchezaji aliyewahi kuandika rekodi hiyo.
Nyota huyo aliyetangaza kuachana na Klabu ya Liverpool ya Ligi Kuu ya England baada ya msimu wa 2025-2026, kumalizika ameandika pia rekodi nyingine ya kuchangia mabao matatu katika fainali za Kombe la Dunia.
Katika fainali za Kombe la Dunia la mwaka 2018, lililofanyika Russia, nyota huyo aliifungia Misri mabao mawili, akianza na kichapo cha 3-1, dhidi ya wenyeji wa michuano hiyo Russia, Juni 19, 2018.
Bao lingine la Salah alilifunga pia katika kichapo cha timu hiyo cha mabao 2-1, dhidi ya Saudi Arabia Juni 25, 2018 na asisiti ya leo mbele ya Ubelgiji imemfanya nyota huyo kuhusika na jumla ya mabao matatu kwenye fainali za Kombe la Dunia linalofanyika nchi za Marekani, Mexico na Canada.