Salah aambiwa baki Liverpool

Muktasari:
- Huu unaweza kuwa msimu wa mwisho kwa Mo Salah, 32, kikosini Anfield kutokana na mkataba wake kufika tamati na hakuna maendeleo mazuri kuhusu mazungumzo ya dili jipya.
LIVERPOOL, ENGLAND: SUPASTAA wa Liverpool, Mohamed Salah ametakiwa kutoshawishika na ofa za klabu za Saudi Arabia, badala yake abaki Liverpool atengeneze hadhi na heshima hata kama atashinda mataji ya Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Huu unaweza kuwa msimu wa mwisho kwa Mo Salah, 32, kikosini Anfield kutokana na mkataba wake kufika tamati na hakuna maendeleo mazuri kuhusu mazungumzo ya dili jipya.
Liverpool itakuwa na uamuzi mgumu wa kufanya ndani ya miezi michache ijayo kutokana na wachezaji wake wengine wawili, Trent Alexander-Arnold na Virgil van Dijk nao kuwa kama Salah, mikataba inakwisha.
Lakini, kocha Diaa El-Sayed, aliyemnoa Salah kwenye timu ya U-20 ya Misri 2011 ambaye ndiye aliyembadili kutoka kuwa beki wa kushoto hadi kuwa fowadi matata, alisema kila mtu kwao Misri anaishabikia Liverpool kwa sababu ya Mo Salah, hivyo angependa kuona anamaliza maisha yake ya soka kama mchezaji akiwa kwenye kikosi hicho cha Merseyside.
Kocha huyo alisema: “Namfahamu Salah tangu alipokuwa mdogo na nafahamu jinsi alivyo na moyo mzuri. Amekuwa na miaka saba matata Liverpool, namba zake zinajieleza.
“Nyakati zake kwenye timu ni moto, wachezaji wenzake, makocha anaofanya nao kazi, waandishi wa habari na mashabiki. Nataka abaki Liverpool. Sisi kule Misri tunamtaka abaki asiondoke. Sitaki kusikia amekwenda Saudi Arabia, PSG au kwenye klabu nyingine. Kwa sababu yake, tunaifuatilia Liverpool.”
Salah ni kinara wa mabao wa Ligi Kuu England msimu huu, akitikisa nyavu mara 25 katika mechi 28 alizocheza na hivyo kupanda hadi namba tatu kwenye wafungaji wa muda wote Liverpool, akifunga mara 131 mechi 241.