Saka mzuka, Martinelli freshi Arteta apata matumaini
Muktasari:
- Mastaa hao wanaweza kurudi uwanjani kwenye mechi ya Fulham, itakayopigwa Jumanne, Aprili 1, kitu ambacho kinaongeza mzuka kwenye kikosi cha Arsenal kinachochuana kwenye mbio za ubingwa msimu huu.
LONDON, ENGLAND: KOCHA, Mikel Arteta amepata mzuka baada ya kupata matumaini Bukayo Saka na Gabriel Martinelli watarejea kwenye kikosi chake cha Arsenal baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa.
Mastaa hao wanaweza kurudi uwanjani kwenye mechi ya Fulham, itakayopigwa Jumanne, Aprili 1, kitu ambacho kinaongeza mzuka kwenye kikosi cha Arsenal kinachochuana kwenye mbio za ubingwa msimu huu.
Kwa maana hiyo, Arsenal itacheza bila ya huduma ya wachezaji hao kwenye mechi sita zijazo, lakini imani ni watarejea mazoezini kwenye kipindi hicho ili kuwa vizuri kwa ajili ya mechi za mwisho za msimu.
Winga wa Arsenal, Martinelli alipatwa na maumivu ya misuli ya paja kwenye nusu fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Newcastle United.
Alikuwapo kwenye kambi ya timu hiyo huko Dubai na maendeleo yake si mabaya, akiwa kwenye hatua za mwisho kurudi uwanjani kuokoa jahazi kwenye timu hiyo yenye majeruhi wengi.
Saka alifanyiwa upasuaji kutokana na maumivu ya misuli ya nyuma ya paja Desemba mwaka jana na hivi karibuni alionekana akijifua kwenye mazoezi ya gym ili kujiweka sawa.
Mwanzoni iliaminika angerejea uwanjani mwezi huu kabla ya kudaiwa atakuwa fiti mwezi ujao.
Lakini, kwa uhakika kabisa wa Saka ni atakuwa fiti kutumika kwenye mechi baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa mwezi ujao, kati Machi 21 na Machi 24.
Kurejea kwa Saka na Martinelli kutakuwa na ahueni kubwa kwa kocha Arteta, ambaye atawakosa kwa msimu wote washambuliaji wake Gabriel Jesus na Kai Havertz, jambo lililomfanya amtumie Raheem Sterling kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati kwenye mechi iliyopita dhidi ya Leicester City kabla ya kumwingiza kiungo Mikel Merino kwenye nafasi hiyo, ambaye alifunga mara mbili kwenye ushindi wa 2-0.
Saka na Martinelli watarudi kwenye kikosi cha Arsenal wakati mwafaka na timu hiyo itakuwa kwenye mapambano ya kusaka ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya endapo kama itavuka na kufika robo fainali.
Wakati huo huo, Arsenal imekumbana na adhabu ya faini ya Pauni 65,000 baada ya wachezaji wao kumzonga mwamuzi kutokana na kadi nyekundu aliyoonyeshwa Myles Lewis-Skelly kwenye mechi dhidi ya Wolves.