Hispania yalipa kisasi baada ya miaka 40, ikiitupa nje Ubelgiji
Muktasari:
- Mechi hiyo ya robo fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Los Angeles, uliopo Jiji la Inglewood katika Jimbo la California, Hispania ilifunga bao la kwanza dakika ya 30, kupitia kiungo, Fabian Ruiz aliyemalizia vizuri mpira uliotemwa na kipa wa Ubelgiji, Thibaut Courtois.
CALIFORNIA, MAREKANI: TIMU ya taifa ya Hispania imefuzu hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia 2026, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ubelgiji.
Mechi hiyo ya robo fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Los Angeles, uliopo Jiji la Inglewood katika Jimbo la California, Hispania ilifunga bao la kwanza dakika ya 30, kupitia kiungo, Fabian Ruiz aliyemalizia vizuri mpira uliotemwa na kipa wa Ubelgiji, Thibaut Courtois.
Wakati Ubelgiji ikicheza kwa tahadhari kubwa, ilisawazisha bao hilo dakika ya 41, mfungaji akiwa Charles De Ketelaere aliyefunga kwa kichwa akimalizia krosi ya Timothy Castagne na kufanya timu hizo kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza kwa sare ya bao 1-1, licha ya Hispania kutawala zaidi kitakwimu.
Bao la Charles De Ketelaere limevunja rekodi ya kipa wa Hispania, Unai Simon ambaye tangu michuano hii ya Kombe la Dunia 2026, imeanza alikuwa hajaruhusu bao lolote katika dakika 649, alizochezea kikosi hicho.
Kipindi cha pili kilianza kwa Hispania kuendelea kulishambulia zaidi lango la Ubelgiji, ambapo dakika ya 88, ilipata bao la pili kupitia Mikel Merino aliyemalizia mpira uliomshinda kipa, Senne Lammens aliyeingia kuchukua nafasi ya Courtois aliyeumia.
Merino alitumia dakika mbili kufunga bao hilo baada ya kuingia dakika ya 86, akichukua nafasi ya Dani Olmo ikiwa ni mwendelezo wa kiwango bora kwa nyota huyo kufuatia kufunga bao pekee dhidi ya Ureno katika hatua ya 16 bora.
Ushindi huu ni wa kisasi kwa Hispania kwani kabla ya leo mara ya mwisho kukutana na Ubelgiji katika hatua ya robo fainali ilichapwa kwa penalti 5-4, Juni 22, 1986, baada ya sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 120, kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia zilizofanyika Mexico.
Hata hivyo, timu hizo zilikutana tena katika hatua ya makundi ya kundi E ya Kombe la Dunia mwaka 1990 nchini Italia, ambapo Hispania ililipa pia kisasi kwa kuifunga Ubelgiji mabao 2-1, mechi iliyopigwa Juni 21, 1990.
Kwa matokeo haya Hispania imefuzu hatua ya nusu fainali na sasa itakutana na Ufaransa iliyofuzu baada ya kuifunga Morocco kwa mabao 2-0, katika mechi iliyopigwa Julai 9, 2026.
Katika mechi hiyo kali na ya kuvutia ya nusu fainali inayosubiriwa zaidi na mashabiki wengi wa soka duniani kati ya Ufaransa dhidi ya Hispania, itachezwa Jumanne ya Julai 14, 2026, kwenye Uwanja wa Dallas, uliopo mji wa Arlington katika Jimbo la Texas, Marekani.
Hispania ilifika hatua ya robo fainali baada ya kuichapa Ureno kwa bao 1-0, huku kwa upande wa Ubelgiji ikiitoa waandaaji wenza wa fainali za Kombe la Dunia la mwaka 2026, timu ya taifa ya Marekani kwa kuifunga mabao 4-1.
Hispania ni moja ya timu kubwa za Ulaya katika soka la kimataifa na historia ya kikosi hicho kwenye Kombe la Dunia ina mafanikio makubwa na changamoto nyingi mbalimbali kabla ya kupata ubingwa wao wa kwanza mwaka 2010, nchini Afrika ya Kusini.
Timu hiyo inashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya 17, tangu ilipoanza mwaka 1934, 1950, 1962, 1966, 1978, 1982, 1986, 1990, 1994, 1998, 2002, 2006, 2010, 2014, 2018, 2022 na sasa 2026, ikiwa ni miongoni pia mwa taifa kubwa Ulaya kisoka.
Mbali na ubingwa wao wa kwanza mwaka 2010, iliouchukua nchini Afrika Kusini baada ya kuifunga Uholanzi bao 1-0, Julai 11, 2010, mafanikio mengine ya Hispania ni kumaliza nafasi ya nne katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1950, nchini Brazil.
Kwa upande wa Ubelgiji, ina historia ya muda mrefu katika Kombe la Dunia, licha ya vipindi vya mafanikio na changamoto tofauti, ikishiriki mara 15, kuanzia 1930, 1934, 1938, 1954, 1970, 1982, 1986, 1990, 1994, 1998, 2002, 2014, 2018, 2022 na sasa 2026.
Mafanikio bora zaidi ni ya kumaliza nafasi ya tatu katika fainali za 2018, zilizofanyika Urusi, baada ya kuifunga England mabao 2-0, yaliyofungwa na Thomas Meunier na Eden Hazard katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Saint Petersburg, Julai 14, 2018.
Pia, ilifika hadi nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1986, nchini Mexico na kuchapwa na Argentina mabao 2-0, yaliyofungwa yote na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Diego Maradona Juni 25, 1986, aliyeipa taji timu hiyo mwaka huo baada ya kuifunga Ujerumani Magharibi mabao 3-2.