Saka asaini mkataba mpya Arsenal, kulipwa kibosi
Muktasari:
- Mkataba wake wa awali ulikuwa unamalizika 2027, lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 sasa ameongeza muda wake, hatua ambayo huenda ikamfanya atumie miaka yake bora zaidi Kaskazini mwa London.
LONDON, ENGLAND: HABARI ndo hiyo. Bukayo Saka amesaini mkataba mpya wa miaka mitano kwenye klabu ya Arsenal na kumfanya kuwa mchezaji anayelipwa zaidi katika kikosi hicho chenye maskani yake Emirates.
Dili hilo jipya litamfanya Saka aendelee kukipiga katika kikosi cha Arsenal hadi 2031. Na kinachoelezwa ni kwamba mkataba huo mpya wa Saka una thamani ya Pauni 78 milioni, ambapo utashuhudiwa mkali huyo wa kimataifa wa England akilipwa Pauni 300,000 kwa wiki.
Mkataba wake wa awali ulikuwa unamalizika 2027, lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 sasa ameongeza muda wake, hatua ambayo huenda ikamfanya atumie miaka yake bora zaidi Kaskazini mwa London.
Akiwa ni zao la akademi ya Hale End, Saka amekuwa nguzo muhimu katika mafanikio ya hivi karibuni ya Arsenal, yaliyowafanya kumaliza katika nafasi ya pili kwa misimu mitatu mfululizo. Winga huyo mwenye kipaji anatarajiwa kufikisha mechi yake ya 300 akiwa na kikosi cha wakubwa cha Arsenal msimu huu, akiwa tayari amehusika katika mabao 155 katika mechi 296 alizocheza hadi sasa akifunga mabao 77 na kutoa pasi za mabao 78.
Saka anaungana na orodha ndefu ya wachezaji waliosaini mikataba mipya katika kikosi hicho kinachonolewa na Mhispaniola, Mikel Arteta.
William Saliba, Gabriel Magalhaes, Ethan Nwaneri na Myles Lewis-Skelly wote walisaini mikataba ya muda mrefu majira ya kiangazi, huku chipukizi wa akademi Max Dowman akikubaliana na masharti ya ufadhili pamoja na makubaliano ya awali kabla ya kutimiza miaka 17, Desemba.
Kujitolea kwa Saka kutampa nguvu kocha Arteta wakati kikosi chake kikionekana kuwa karibu zaidi kuwahi kutwaa taji lao la kwanza la Ligi Kuu England katika kipindi cha miaka 22 na pengine kutimiza historia kwa kushinda mataji manne.
Arsenal, ambayo ilitarajiwa kukutana na Wolves usiku wa Jumatano, ilikuwa mbele kwa pointi nne kileleni mwa msimamo wa ligi na ilikuwa na nafasi ya kutanua zaidi pengo hilo la pointi huku kikosi hicho kikifuzu pia raundi ya tano ya Kombe la FA, fainali ya Carabao Cup na imetinga kwenye hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mkataba mpya unaweza pia kuambatana na nafasi mpya kwa Saka, ambaye alijaribiwa kucheza eneo la kati katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Wigan kwenye Kombe la FA, Jumapili iliyopita.
Kutokana na Arsenal kuwa na matatizo ya majeruhi wengi kwenye kikosi chao kama Mikel Merino, Martin Odegaard na Kai Havertz, Arteta alisema anaweza kuendelea kumtumia Saka katika nafasi ya Namba 10, aliposema: "Kwa sasa tuna matatizo ya viungo na wachezaji wanaingia kuziba mapengo. Bukayo aliingia na suala lake ni jambo tunalopaswa kulizingatia kwa siku zijazo, lakini ni jambo jema sana, hasa namna ambavyo wachezaji wanavyoitikia majukumu tofauti kwa mtazamo mzuri."
Aliongeza: "Nadhani anafurahia kucheza Namba 10 na kila kitu kinachomletea changamoto. Chochote kinachompa nafasi ya kujithibitisha, humchochea zaidi na nadhani hilo ni jambo chanya."
MASTAA 10 WENYE
MISHAHARA MIKUBWA
ARSENAL KWA WIKI
1.Bukayo Saka - Pauni 300,000+
2.Kai Havertz - Pauni 275,000
3.William Saliba - Pauni 250,000
4.Declan Rice - Pauni 225,000
5.Martin Odegaard - Pauni 220,000
6.Gabriel Jesus - Pauni 220,000
7.Viktor Gyokeres - Pauni 200,000
8.Gabriel Martinelli - Pauni 180,000
9.Eberechi Eze - Pauni 175,000
10.Gabriel Magalhaes - Pauni 150,000