Arsenal kuna kitu! Havertz kukosa mechi muhimu
Muktasari:
- Awali, aliumia dhidi ya Manchester United, hali iliyomlazimu kufanyiwa upasuaji mdogo na baada ya hapo aliporejea, aliongeza machaguo zaidi kwa Arteta katika safu ya ushambuliaji.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imepata pigo jingine katika harakati zakeza kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England na michuano mbalimbali baada ya mshambuliaji wake Kai Havertz kukabiliwa na tatizo la misuli litakalomuweka nje ya uwanja kwa muda, wakati huu ambapo michezo muhimu inakaribia.
Kwa mujibu wa tovuti ya The Athletic, mshambuliaji huyo raia wa Ujerumani hatakuwepo kwenye Dabi ya Kaskazini mwa London dhidi ya Tottenham, pamoja na mechi dhidi ya Brentford, Wolves na Wigan.
Hii sio mara ya kwanza kwa Havertz kuumia msimu huu, aliwahi pia kukosa sehemu kubwa ya nusu ya kwanza ya msimu kutokana na jeraha la goti.
Awali, aliumia dhidi ya Manchester United, hali iliyomlazimu kufanyiwa upasuaji mdogo na baada ya hapo aliporejea, aliongeza machaguo zaidi kwa Arteta katika safu ya ushambuliaji.
Mapema msimu huu, Arteta alilazimika kumtegemea Viktor Gyokeres, wakati Gabriel Jesus akiendelea kupona jeraha la goti, huku kutokuwepo kwa Havertz kukiongeza ugumu.
Havertz amecheza mechi tatu tu za ligi msimu huu, akianza katika michezo miwili ya mwisho dhidi ya Leeds United na Sunderland.
Katika mchezo dhidi ya Sunderland, alitoa pasi ya bao, jambo lililoongeza matumaini kuwa anaweza kusaidia zaidi timu katika mapambano ya ubingwa.
Mechi hiyo dhidi ya Sunderland alichezeshwa katika eneo la kiungo cha kati jambo lililompa Gyokeres uhuru zaidi mbele.
Akieleza sababu ya kumtumia Havertz katika nafasi hiyo, Arteta amesema:
“Nilihisi kutokana na aina ya mchezo ambao Sunderland inaucheza. Niliona nimtumie kwa sababu Kai ana sifa tofauti sana ukilinganisha na Martin, Ebs au kiungo mwingine mshambuliaji.”
Baada ya Man City kuibuka na ushindi juzi mbele ya Fulham, imesababisha tofauti ya alama kati yao na Arsenal ipungue kufikia tatu ingawa washika mitutu hao walicheza usiku wa kuamkia leo.
Havertz anaungana na orodha ya mastaa wengine wanaosumbuliwa na majeraha ikiwa pamoja na Mikel Merino ambaye amevunjika mfupa wa mguu na atakuwa nje kwa muda mrefu.
Pia kuna sintofahamu juu ya hali za Bukayo Saka, Martin Odegaard na Leandro Trossard, ambao wanasumbuliwa na majeraha madogo madogo.