Saka anavyoleta machaguo mengi Arsenal
Muktasari:
- Bukayo Saka siku zote alikuwa mhimili katika harakati za Arsenal kutwaa Ligi Kuu England, lakini hakuna aliyedhani kwamba angekuwa mhimili huo katikati ya uwanja.
LONDON, ENGLAND: DIRISHA la usajili lilifungwa wiki mbili zilizopita, lakini Mikel Arteta ghafla amepata silaha mpya.
Bukayo Saka siku zote alikuwa mhimili katika harakati za Arsenal kutwaa Ligi Kuu England, lakini hakuna aliyedhani kwamba angekuwa mhimili huo katikati ya uwanja.
Lakini, ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Wigan Athletic katika Kombe la FA, Jumapili umempa Arteta jambo la kutafakari kadri mechi za mwisho wa msimu zinavyoanza.
Saka aliondolewa kwenye nafasi ya kawaida ya winga wa kulia na kuvutia wengi alipopangwa kiungo mshambuliaji (No.10). Mabadiliko hayo yalilazimishwa baada ya Riccardo Calafiori kuumia wakati wa kupasha misuli na Myles Lewis-Skelly kuhamishiwa beki wa kushoto. Saka aliingizwa kikosini dakika za mwisho na kuiongoza timu kama nahodha akiwa katikati ya uwanja.
Arteta mara nyingi huzungumzia kuwa mgumu kutabirika katika uchaguzi wa kikosi na huu ulikuwa mfano halisi. Ni mbinu gani kubwa zaidi kuliko kumhamisha mchezaji wako nyota kutoka nafasi yake ya kawaida? Sasa makocha wapinzani watakuwa wanajiuliza kama Arteta atafanya hivyo tena na bila shaka atashawishika kufanya hivyo.
Saka alipoteza pasi moja tu kati ya pasi 26 alizopiga dhidi ya Wigan, huku Christian Norgaard na William Saliba pekee wakimpita kwa kurejesha mipira mingi zaidi. Nyota huyo wa England alifanya yote hayo licha ya kutolewa mapema kipindi cha pili kama ilivyopangwa.
Arteta tayari alikuwa akiangalia mbele kwenye safari ngumu dhidi ya Wolves, ambapo ushindi utaifanya Arsenal kuongoza kwa pointi saba dhidi ya Manchester City kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England. Kutokana na masuala ya utimamu wa mwili, Saka ni chaguo halisi kubaki katikati kwa mechi hiyo na hata safari ya Jumapili kumenyana na Tottenham Hotspur.
Arsenal haitakuwa na Kai Havertz na Mikel Merino kutokana na majeraha. Nahodha Martin Odegaard ana shaka kutokana na tatizo la goti, hali inayomwacha Eberechi Eze kama chaguo jingine la kiungo mshambuliaji. Arteta alisema: “Hilo linawezekana. Nilitaka kujaribu na tunaweza kulitumia tena siku zijazo. Bado tuna mechi nyingi na mashindano tofauti msimu huu na hilo ni chaguo tulilonalo.”
Arteta alipoulizwa anapenda nini Saka anapocheza katikati, alisema: “Yuko karibu zaidi na lango. Ni vigumu kwa mpinzani kumfuatilia kila wakati. Anaweza kubadilishana nafasi na winga, na ni mzuri kutafuta nafasi. Akiwa hapo, anaweza kukuumiza sana akiwa na mpira.”
Kutokana na hilo, Arteta sasa anaweza kumtumia Saka kwenye machaguo matatu tofauti.
1. Kiungo Namba 10; Arteta anaweza kumchezesha Saka kama No.10 wa pekee mbele ya Declan Rice na Martin Zubimendi. Hii itampa uhuru mkubwa wa kushambulia, huku nyuma yake kukiwa na viungo wawili imara wanaoweza pia kusaidia mashambulizi.
2. Namba 8 wa kulia; Saka amezoea kucheza katika nusu ya kulia ya uwanja. Akiwekwa kama No.8 wa kulia, ataendelea kutumia maeneo anayoyajua vizuri huku akiwa na uhuru wa kuingia katikati kuathiri mchezo. Hii pia itamruhusu Madueke kubaki winga wa kulia, wakitumia maelewano yao mazuri. Rice anaweza kucheza kama Namba 8 wa kushoto, huku Zubimendi akiwa nyuma kama kiungo mkabaji.
3. Namba 8 wa kushoto; Arteta anaweza kumchezesha Saka kama Namba 8 wa kushoto, akimpandisha Eze mbele zaidi na kumwacha Rice kama Namba 6 wa pekee.