Rooney: Tuanze upyaa

Muktasari:
- Rooney alitoa kauli hiyo baada ya kumtaja mwekezaji mwenza wa Man United, Sir Jim Ratcliffe, alivyosema waziwazi kuhusu ubora wa kikosi cha sasa.
MANCHESTER, ENGLAND: LEJENDI wa Manchester United, Wayne Rooney, amedai kwamba timu hiyo inahitaji kufanya "mabadiliko makubwa" ili kupata mafanikio, akiamini kikosi cha sasa hakina kiwango cha kuwafikisha nchi ya ahadi.
Rooney alitoa kauli hiyo baada ya kumtaja mwekezaji mwenza wa Man United, Sir Jim Ratcliffe, alivyosema waziwazi kuhusu ubora wa kikosi cha sasa.
Katika mfululizo wa mahojiano Jumatatu, Ratcliffe alisema baadhi ya wachezaji wa sasa ni "wanalipwa pesa nyingi na hawana viwango".
Bilionea huyo kutoka kampuni ya Ineos alitaja wachezaji kama Jadon Sancho, Rasmus Hojlund, Casemiro, Antony, na Andre Onana, akisema kuwa Man United bado wanadaiwa fedha kwa usajili wa wachezaji hao wa gharama kubwa.
Kauli za Ratcliffe zinakuja katika kipindi hiki ambacho Man United inashika nafasi ya 14 katika msimamo wa Ligi Kuu England huku taji pekee ambalo wanaonekana kuwa wanaweza kulipata ni Europa League.
Rooney ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa Man United, alisema haoni kama kikosi cha sasa kinaweza kuisaidia Man United.
Akizungumza kupitia podcast ya 'Stick to Football', Rooney alisema, "Hapana, sidhani kama wanaweza kuifikisha timu pazuri. Wanakosa mwelekeo, wanashindwa, wanahofu."
"Bruno Fernandes ndiye mchezaji anayeendelea kutoa kiwango bora, kuna muda naye huwa anakera lakini bado anaonyesha uwezo. Timu inahitaji mabadiliko makubwa katika kikosi, nafikiri wachezaji 10 hadi 15 wanapaswa kuondoka klabuni. Kingine, ningemwacha Bruno na Kobbie Mainoo."
"Kumekuwa na tamaduni katika timu kwa sasa ambapo inakuwa rahisi kupoteza michezo na wachezaji wanatoka na kusema, 'Tunaenda kufanya vizuri mechi inayofuata,' hayo ni maneno yote yasiyofaa, onyesha hali ya kupigana uwanjani."
"Inasikitisha kutazama, inaniuma. Mimi natokea Jiji la Liverpool lakini nilitumia miaka mingi Man United, nataka timu ifanye vizuri, sina watoto katika akademi ila inaniuma kuona wanavyocheza."
Kocha wa Man United, Ruben Amorim, alikiri kabla ya mechi ya Europa League dhidi ya Real Sociedad kuwa kikosi chake hakiwezi kufanya vizuri.