Rooney amkosoa Kane, rekodi zikivunjwa Ulaya
Muktasari:
- Mchezo huo wa nusu fainali umeingia kwenye historia ya mashindano hayo, ukiwa miongoni mwa michezo yenye mabao mengi zaidi kuwahi kuchezwa katika hatua hiyo tangu Eintracht Frankfurt walipoifunga Rangers mabao 6-3 msimu wa 1959-60.
PARIS, UFARANSA: NYOTA wa zamani wa Manchester United, Wayne Rooney, amemkosoa Harry Kane baada ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku wa Jumanne iliyomalizika kwa Paris Saint-Germain kuibuka na ushindi wa mabao 5-4 dhidi ya Bayern Munich kwenye Uwanja wa Parc des Princes, Ufaransa.
Mchezo huo wa nusu fainali umeingia kwenye historia ya mashindano hayo, ukiwa miongoni mwa michezo yenye mabao mengi zaidi kuwahi kuchezwa katika hatua hiyo tangu Eintracht Frankfurt walipoifunga Rangers mabao 6-3 msimu wa 1959-60.
Pia hii ni mara ya kwanza katika historia ya nusu fainali ya michuano mikubwa ya Ulaya kwa timu zote mbili kufunga angalau mabao manne kila mmoja.
Kwa upande wa msimu huu, mechi hiyo pia imeweka alama nyingine ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu mbili kukutana katika nusu fainali huku kila moja ikiwa tayari imefunga zaidi ya mabao 40 katika msimu mmoja wa Ligi ya Mabingwa.
Licha ya burudani hiyo, Harry Kane aliyefunga bao la kwanza kwa penalti alisema; “Hata kama kulikuwa na mabao tisa, kulikuwa na ulinzi mzuri sana hasa kwenye mapambano ya ana kwa ana (mchezaji kwa mchezaji).”
Lakini kauli hiyo haikumvutia Rooney na badala yake alipinga mtazamo huo kwa kusema; “Nampenda Kane, lakini hakuna namna anaweza kuwasifia mabeki wake baada ya mechi kama hii. Ulinzi wa timu zote ulikuwa hovyo sana.”
Katika mechi hiyo, safu ya ulinzi ya Bayern iliyojumuisha Jonathan Tah, Dayot Upamecano, Alphonso Davies na Josip Stanisic ilipata wakati mgumu dhidi ya mashambulizi ya PSG yakiongozwa na Ousmane Dembele.
Kwa upande mwingine, nguli wa soka Thierry Henry alieleza kuwa burudani ndiyo muhimu zaidi kuliko makosa ya ulinzi.
“Tumekuwa tukilalamika soka limekuwa la kuchosha, lakini mechi kama hii inaonyesha uzuri wa mchezo huu,” alisema.
Mbali na rekodi za pamoja ambazo ziliwekwa usiku huo, Kane naye aliweka rekodi binafsi kwa kufunga katika mechi sita mfululizo za Ligi ya Mabingwa Ulaya, akivunja rekodi ya Steven Gerrard.
Sasa macho ya wengi yanaelekezwa kwenye mchezo wa marudiano utakaochezwa Munich ambapo Bayern Munich watakuwa na kazi kubwa ya kugeuza matokeo dhidi ya Paris Saint-Germain ili kufuzu fainali, watakayokutana na mshindi kati ya Atletico Madrid na Arsenal.