Ronaldo na kilio cha mtu mzima
Muktasari:
- Cristiano Ronaldo amekiri kuwa hili lilikuwa Kombe lake la Dunia la mwisho, lakini hajakata tamaa ya kuendelea kuitumikia timu ya taifa ya Ureno.
MIAMI, Marekani: 'UKIONA mtu mzima analia mbele za watu ujue kuna jambo...' Ndicho kilichoonekana kwa chozi la mshambuliaji wa Cristiano Ronaldo baada ya kukiri hili ilikuwa Kombe lake la Dunia la mwisho, lakini hajafunga mlango wa kuendelea kuichezea Ureno.
Cristiano Ronaldo amekiri kuwa hili lilikuwa Kombe lake la Dunia la mwisho, lakini hajakata tamaa ya kuendelea kuitumikia timu ya taifa ya Ureno.
Na huku michuano ya Mataifa ya Ulaya yajayo yakitarajiwa kufanyika baada ya miaka miwili, kauli zake zimezua mjadala kuhusu uwezekano wa mshindi huyo mara tano wa tuzo ya Ballon d'Or kuendelea kucheza hadi Euro 2028, ambapo atakuwa na umri wa miaka 43.
Ronaldo alionekana akilia baada ya Ureno kutolewa kwenye Kombe la Dunia katika hatua ya 16 bora Jumatatu, kufuatia bao la dakika za majeruhi lililofungwa na Mikel Merino na kuipeleka Hispania robo fainali.
Matokeo hayo yanamaanisha kuwa nyota huyo wa zamani wa Real Madrid CF, Manchester United na Juventus FC atamaliza maisha yake ya soka bila kutwaa taji la Kombe la Dunia.
Hilo ndilo taji ambalo mpinzani wake mkubwa, Lionel Messi, tayari analimiliki na sasa anawania kulitwaa kwa mara ya pili akiwa na Argentina.
Hata hivyo, Ronaldo alionyesha msimamo wake wa kawaida alipokuwa akitafakari miaka 23 ya kuitumikia timu ya taifa na kuzungumzia mustakabali wake.
Alisema:"Nina huzuni kuondolewa kwenye Kombe la Dunia kwa namna hii."
"Lakini nilitoa kila kitu nilichokuwa nacho. Nilifanya kila nililoweza. Ninaondoka nikiwa na dhamiri safi."
"Huu ndio mpira wa miguu, haya ndiyo maisha ya mchezaji. Wakati mwingine unashinda, wakati mwingine unapoteza. Lazima uendelee mbele."
"Ukweli ni kwamba hili lilikuwa Kombe langu la Dunia la mwisho, ndiyo. Lakini sasa nitapata muda wa kutafakari, kuwa pamoja na familia yangu na kutofanya uamuzi kwa papara. Maisha lazima yaendelee."
Kauli hiyo ilifuatiwa na maelezo yanayoashiria kuwa bado hajafunga mlango wa kuendelea kuchezea Ureno, huku akieleza mapenzi yake kwa michuano ya Euro, ambayo aliisaidia Ureno kuishinda mwaka 2016 na ambayo anaweza kushiriki tena baada ya miaka miwili.
Aliendelea kusema:"Leo ninajisikia vivyo hivyo. Nina dhamiri safi. Nilitoa kila nilichoweza. Nimeshinda mataji matatu nikiwa na Ureno."
"Kabla ya Cristiano, Ureno haikuwa imeshinda taji lolote. Hivyo nina furaha."
"Kwa kweli, taji kubwa zaidi nililoshinda na timu ya taifa ni lile la mwaka 2016, ambalo kwangu lina thamani sawa na Kombe la Dunia."
"Ndiyo maana narudia kusema, ninaondoka nikiwa na dhamiri safi. Nilifanya kila nilichoweza. Kesho ni siku mpya na maisha yanaendelea."
Ronaldo bado ana mkataba na klabu ya Al-Nassr FC unaomalizika Juni mwakani, wakati atakapokuwa na umri wa miaka 42.
Akiwa ndiye mchezaji aliyeichezea timu ya taifa mara nyingi zaidi na mwenye mabao mengi zaidi katika historia ya soka la kimataifa la wanaume, Ronaldo ameendelea kuvunja rekodi nyingi kiasi kwamba zimebaki chache sana za kufikia.
Kwa sasa amebakiza mabao 24 kufikisha mabao 1,000 katika soka la wakubwa, na inakadiriwa anaweza kufikia rekodi hiyo msimu ujao.
Hata hivyo, kwenye Kombe hili la Dunia alifunga mabao matatu pekee, wakati Lionel Messi akiendelea kuwania Kiatu cha Dhahabu akiwa na mabao saba na bado akiendelea kung'ara akiwa na Argentina.