'Trump Dance' ya Ubelgiji gumzo
Muktasari:
- Wachezaji wa Ubelgiji walimkejeli Rais Donald Trump baada ya kuhusishwa kwake na maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Marekani.
NEW YORK, Marekani: NYOTA wa Ubelgiji baada ya kuichapa Marekani aliamua kufanya utani kwa kucheza "Trump Dance." kwa mtindo wa kucheza muziki wa Rais Donald Trump.
Wachezaji wa Ubelgiji walimkejeli Rais Donald Trump baada ya kuhusishwa kwake na maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Marekani.
Ubelgiji 'Mashetani Wekundu' waliibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya wenyeji wenza wa Kombe la Dunia Marekani mjini Seattle, huku Charles De Ketelaere akifunga mabao mawili katika kipindi cha kwanza.
Hata hivyo, mjadala mkubwa kabla ya mechi ulihusu mazingira tata yaliyomruhusu Folarin Balogun kucheza.
Balogun alikuwa amepewa kadi nyekundu katika ushindi wa Marekani dhidi ya Bosnia and Herzegovina kwenye hatua ya 32 bora, hivyo alitarajiwa kutumikia adhabu ya kutocheza dhidi ya Ubelgiji.
Lakini adhabu hiyo ilifutwa na FIFA baada ya Trump kuripotiwa kumpigia simu Rais wa FIFA, Gianni Infantino.
Uamuzi huo ulizua ukosoaji mkubwa, ukiwemo kutoka Shirikisho la Soka la Ubelgiji na UEFA, ambayo ilisema kuwa chombo hicho cha kusimamia soka duniani "kimevuka mipaka" na kuibua mashaka kuhusu uadilifu wa mchezo.
SunSport iliripoti kuwa Ubelgiji ilikuwa tayari kufungua kesi katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), ili kupinga matokeo endapo ingepoteza dhidi ya Marekani iliyomjumuisha Balogun.
Lakini kama msemo maarufu wa mpira wa kikapu nchini Marekani unavyosema, 'Mpira haudanganyi', Ubelgiji ndiyo iliyocheka mwisho baada ya kuwadhihaki Trump kufuatia sakata hilo la Balogun.
Mshambuliaji wa zamani wa Manchester United na Chelsea F.C., Romelu Lukaku, aliingia akitokea benchi na kufunga bao la nne la timu yake.
Baada ya bao hilo, yeye pamoja na wenzake walisherehekea kwa kuiga staili ya kucheza inayojulikana kama "Trump Dance."
Trump, mwenye umri wa miaka 80, mara nyingi huonekana kwenye mikutano yake ya kisiasa akicheza kwa kusogeza mikono upande kwa upande huku akifanya miondoko midogo ya sehemu ya chini ya mwili.
Lakini baada ya kuifunga timu ya Marekani iliyokuwa chini ya kocha Mauricio Pochettino, ni Wabelgiji waliokuwa wakicheza kwa furaha wakitinga robo fainali.
Mashabiki kwenye mitandao ya kijamii walifurahia kejeli hiyo.
Mmoja aliandika: "Unafungwa 4-1 nyumbani halafu wapinzani wanasherehekea kwa Trump Dance... huo ni utani wa kiwango cha juu kabisa."
Mwingine alisema: "Kejeli ya hali ya juu."
Wa tatu aliandika: "Ubelgiji walicheza Trump Dance baada ya bao lao la nne dhidi yetu. Siwezi kukataa kuwaheshimu kwa utani huo. Walituchapa, wanastahili kucheza."
Mwingine aliongeza: "Hii ni kejeli ya kiwango kingine kabisa."
Marekani ilikuwa timu ya mwisho kati ya mataifa matatu wenyeji iliyosalia kwenye mashindano, baada ya Canada na Mexico kutolewa katika hatua ya 16 bora na Morocco na England mtawalia.
Ushindi huo umeifanya Ubelgiji kufuzu robo fainali, ambako itakutana na Hispania Julai 10, baada ya mabingwa hao wa Ulaya kuiondoa Ureno kwa bao la ushindi lililofungwa katika dakika za majeruhi na Mikel Merino.