Pigo kubwa! Henderson kutemwa Kombe la Dunia
Muktasari:
- Kiungo wa England, Jordan Henderson, anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa kifundo cha mkono alichokiumiza wakati wa kusherehekea ushindi wa timu yake wa mabao 3-2 dhidi ya Mexico katika hatua ya 16 bora, jambo linalotia shaka ushiriki wake katika mechi zilizobaki za Kombe la Dunia.
MIAMI, Marekani: KIUNGO wa England, Jordan Henderson anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa kifundo cha mkono, huku ushiriki wake uliosalia Kombe la Dunia ukitia shaka.
Kiungo wa England, Jordan Henderson, anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa kifundo cha mkono alichokiumiza wakati wa kusherehekea ushindi wa timu yake wa mabao 3-2 dhidi ya Mexico katika hatua ya 16 bora, jambo linalotia shaka ushiriki wake katika mechi zilizobaki za Kombe la Dunia.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36 alionekana kuangukia vibaya baada ya kuruka juu ya mabango ya matangazo kwenye Uwanja Azteca, kabla ya kutolewa nje ya uwanja kwa machela.
Kocha mkuu wa England, Thomas Tuchel, alisema baada ya ushindi huo kwenye mahojiano na BBC One:
"Jordan Henderson alianguka na kuumia kifundo cha mkono. Inaonekana ni jeraha baya sana."
Aliongeza: "Ni jeraha kubwa na halilingani kabisa na furaha ya ushindi wa leo kwa sababu Jordan hayupo pamoja nasi sasa. Daktari amenieleza kuwa yuko hospitalini."
Baada ya mechi ya Jumatatu, Henderson alisindikizwa hadi hospitali mjini Mexico City na mmoja wa maafisa wa benchi la ufundi la England, hivyo hakusafiri pamoja na kikosi kilichorejea katika kambi yao iliyopo Kansas City.
Inaelezwa kuwa kiungo huyo wa Brentford ana hamu ya kuendelea kubaki na kikosi cha England kwa muda wote watakaokuwa nchini Marekani, licha ya uwezekano wa kukosa mechi zilizobaki kutokana na jeraha hilo.