Ronaldo awatibua mashabiki, wamshambulia mtandaoni
Muktasari:
- Nahodha huyo wa Ureno alichukua jukumu la kupiga penalti katika kipindi cha pili, lakini mkwaju wake uliokolewa kwa mguu na mlinda lango wa Ireland, Caoimhin Kelleher.
Baadhi ya mashabiki waliokerwa na hatua ya Cristiano Ronaldo kukosa penalti kwenye mechi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Ireland ya Kaskazini usiku wa kuamkia leo, wamemshambulia mitandaoni mshambuliaji huyo wa klabu ya Al-Nassr.
Nahodha huyo wa Ureno alichukua jukumu la kupiga penalti katika kipindi cha pili, lakini mkwaju wake uliokolewa kwa mguu na mlinda lango wa Ireland, Caoimhin Kelleher.
Wakiwa na hamu ya kuendeleza rekodi yao nzuri katika Kundi F, mabingwa wa Ligi ya Mataifa (Nations League) walianza kwa nguvu. Ronaldo karibu afunge katika dakika ya 17 kwa shuti kali kutoka yadi 20, lakini mpira uligonga mwamba.
Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika bila bao, Ureno iliendelea kushambulia, lakini ngome ya Ireland ikabaki imara, hasa kutokana na mikwaju mingi kuokolewa na Kelleher. Ureno ilipata nafasi kubwa ya kufunga pale Dara O'Shea alipopigwa kwa mpira na Trincao uliogonga mkono wake ndani ya boksi. Hata hivyo, Ronaldo alikosa penalti hiyo muhimu.
Ureno iliongeza kasi katika dakika za mwisho, na juhudi zao zikazaa matunda dakika za majeruhi pale Ruben Neves alipofunga kwa kichwa krosi ya Trincao na kuipa timu hiyo ushindi mwembamba wa bao 1-0.
Licha ya ushindi huo, mashabiki wengi walianza kumshambulia Ronaldo kwa kukosa penalti hiyo. Baadhi ya maoni kwenye mtandao wa X (zamani Twitter) yamesomeka:
“Hata penalti hawezi kufunga? Bado hujachelewa kustaafu.”
— @Anonymous_wa_x
“Bro anatakiwa aache soka kabla soka halijamwacha.”
— @BaldeFan3
Mwingine amehoji uwezo wa Ronaldo kufikia lengo lake la mabao 1,000 baada ya kukosa penalti hiyo:
“Bro bado anaweza kufikisha mabao 1000... ukizingatia hawezi kufunga penalti tena?? Nimehuzunika.”
— @GodswillRed
Mwingine ameandika maneno ya utania kwa kumlinganisha na Erling Haaland, aliyekosa penalti mapema siku hiyo, lakini baadaye akafunga hat-trick katika ushindi wa 5-0 wa Norway dhidi ya Israel:
“Ronaldo alimuona Haaland akikosa penalti akadhani naye anaweza kufanya hivyo. Haaland alijibu kwa kufunga magoli 3 lakini Ronaldo kaenda kimya.”
— @Thebanterboot
Mwingine amesifu uwezo wa Kelleher kwa kusema:
“Duuh, ule ukuta wa Kelleher haukupitika! Ronaldo huwa na barafu kwenye mishipa yake, lakini golikipa wa Ireland alimsoma vizuri.”
— @SathishFirewall
Wengine wameendelea kutoa maoni ya kejeli:
“Hata baada ya kupewa penalti ya huruma bado kakosa.”
— @FinishedBluds
“Mlinda mlango Kelleher amesema, ‘Siyo leo Ronaldo!’”
— @icecyclone
Licha ya presha na lawama, mashabiki wengine wanaamini kuwa Ronaldo bado ana nafasi ya kudhihirisha uwezo wake, kwani bado kuna mechi nyingine za kimataifa katika siku za usoni.