Hotuba ya AI, Cristiano Ronaldo ajitetea
Muktasari:
- Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40, ambaye amewahi kutamba katika klabuza Sporting CP, Manchester United, Real Madrid, Juventus na sasa Al-Nassr ya Saudi Arabia, amekuwa akijulikana kwa utulivu na uzoefu mkubwa lakini safari hii, alihisi kuwa anahitaji msaada wa ziada.
LISBON, URENO: NYOTA wa soka duniani Cristiano Ronaldo amekiri kutumia teknolojia ya akili bandia (AI) kuandaa hotuba yake katika hafla ya utoaji tuzo za Portugal Football Globes, baada ya kupokea tuzo maalum ya Globe Prestige Award.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40, ambaye amewahi kutamba katika klabuza Sporting CP, Manchester United, Real Madrid, Juventus na sasa Al-Nassr ya Saudi Arabia, amekuwa akijulikana kwa utulivu na uzoefu mkubwa lakini safari hii, alihisi kuwa anahitaji msaada wa ziada.
Licha ya kuwa amefanikiwa sana katika ulimwengu wa soka, Ronaldo amekiri kwamba kuongea mbele ya hadhira bado humfanya kuwa na hofu kidogo. Katika tukio lisilotarajiwa, mshindi wa Ballon d’Or mara tano alifichua kuwa alitumia teknolojia ya AI kusaidia kuandaa hotuba yake ya kupokea tuzo.
Ronaldo amesema alipokuwa akijiandaa kutoa hotuba yake, alijisikia hana cha kusema, hivyo akaamua kutumia Perplexity, jukwaa la akili bandia linalosaidia kupata taarifa na kuandika maandishi.
Ronaldo ameeleza: “Nina mataji kadhaa nyumbani, lakini hii ni ya kipekee na nzuri. Nilikuwa mezani nikijiuliza, ‘Nitasema nini kwenye hotuba hii?’ Nilijiuliza, ‘Tuzo ya Prestige ni nini hasa? Je, ni tuzo ya kumaliza kazi?’ Nikawa na wasiwasi kidogo na nikasema, ‘Haiwezekani.’
“Kwa hiyo nikafanya utafiti kidogo kupitia Perplexity. Kama hujui ni nini, tafuta ujue. Nilipata msaada kidogo huko.”
Ronaldo amesisitiza kwamba safari yake bado haijaisha, akisema kuwa bado ana ndoto ya kushinda Kombe la Dunia la 2026 akiwa na Ureno, baada ya mafanikio yao kwenye UEFA Nations League ya 2025.
“Tuzo hii ni chanzo cha fahari kubwa kwangu,” amesema.
“Siichukulii kama mwisho wa kazi yangu, bali kama mwendelezo wa kila kitu nilichofanya katika maisha yangu ya soka.”
Kwa mara nyingine, Ronaldo ameonyesha kuwa hata akiwa mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani, bado hana aibu ya kujifunza na kutumia teknolojia mpya akithibitisha kuwa hata mashujaa wanaweza kutegemea AI kidogo wakati wa wasiwasi.