Roberto Martinez: Ronaldo ni mfano wa kuigwa, anajua anachokifanya
Muktasari:
- Martinez amempongeza Ronaldo kwa uwezo na juhudi zake za kupambana wakati wote, hali ambayo ameitaja kama ushawishi kwa wachezaji wengine wa timu ya taifa ya Ureno na wale wanaochipukia kwa ajili ya baadaye.
Kocha wa timu ya taifa ya Ureno, Roberto Martinez, amemwagia sifa nahodha na mshambuliaji wa kikosi chake, Cristiano Ronaldo, kuelekea mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Ireland na Hungary.
Martinez amempongeza Ronaldo kwa uwezo na juhudi zake za kupambana wakati wote, hali ambayo ameitaja kama ushawishi kwa wachezaji wengine wa timu ya taifa ya Ureno na wale wanaochipukia kwa ajili ya baadaye.
Kocha huyo raia wa Hispania, amemzungumzia Ronaldo kwa maneno ya heshima, akimuita mwanasoka wa kipekee.
“Cristiano ni mmoja wa watu wanaotafuta kila jambo dogo linaloweza kuwapa faida au kuwasaidia wengine matatizo kwa haraka zaidi na hilo ni mfano mzuri sana.
"Zaidi ya hayo, ana mapenzi ya kweli na timu ya taifa. Kwa benchi la ufundi, hakuna jambo zuri zaidi kuliko kuona mchezaji anayejivunia kuiwakilisha nchi yake.
"Unapomuona mtu kama huyo ambaye ndiye mchezaji pekee duniani aliyewahi kucheza mechi zaidi ya 200 za kimataifa, unajua ni mfano wa kuigwa,” amesema.
Jumamosi Oktoba 11, 2025, Ureno itacheza dhidi ya Ireland, kisha Oktoba 14, 2025 itakutana na Hungary.
Baada ya kutunukiwa tuzo ya Globo Prestigio kwenye hafla ya Portugal Football Globes, Cristiano Ronaldo alifunguka kuhusu namna anavyothamini kuvaa jezi ya timu ya taifa ya Ureno. Amesema kama ingewezekana, angeacha kabisa soka la klabu ili achezee Ureno pekee.
Akiwa na umri wa miaka 40, Cristiano Ronaldo bado anaendelea kuthibitisha kuwa yeye ni sehemu muhimu ya timu ya taifa ya Ureno.
Mshindi huyo wa tuzo ya Ballon d'Or mara tano alitunukiwa tuzo ya ‘Best of All Time’ na Ligi ya Ureno mwezi uliopita, na hivi karibuni pia alipokea tuzo ya Globo Prestigio, ikitambua miaka 22 ya kuichezea Ureno katika ngazi ya kimataifa.