Ronaldo atafuta timu Kombe la Dunia

Muktasari:
- Ronaldo, 40, mkataba wake kwenye klabu hiyo ya Saudi Arabia utafika ukomo dirisha hili la majira ya kiangazi
RIYADH, SAUDI ARABIA: SUPASTAA Cristiano Ronaldo amethibitisha kwamba ataachana na Al Nassr kupitia posti yake kwenye mtandao wa kijamii.
Ronaldo, 40, mkataba wake kwenye klabu hiyo ya Saudi Arabia utafika ukomo dirisha hili la majira ya kiangazi. Na kinachoonekana nyakati zake za kucheza kwenye Saudi Pro League zimefika kikomo kwa posti yake aliyoposti Instagram: “Huu ukurasa umeshafungwa. Stori? Bado inaandikwa. Nawashukuru nyote.”
Rais wa Fifa, Gianni Infantino alithibitisha wiki iliyopita kwamba Ronaldo yupo kwenye mazungumzo ya kujiunga na moja ya klabu itakayoshiriki kwenye Kombe la Dunia la Klabu. Michuano hiyo itaanza Juni 14 huko Marekani. Infantino alisema: “Ronaldo anaweza kucheza moja ya timu zitakazoshiriki Kombe la Dunia la Klabu. Yupo kwenye mazungumzo na baadhi ya klabu, hivyo kama kuna timu inamfuatilia na ipo kwenye mpango wa kumchukua kwa ajili ya Kombe la Dunia la Klabu, huwezi kujua, nani anajua.”
CR7 amekuwa akihusishwa na moja ya klabu huko Brazil, ambayo itakwenda kwenye fainali hizo za Marekani. Palmeiras, Flamengo, Fluminense na Botafogo ni timu nne za Brazil, ambazo zitakwenda kushiriki fainali hizo zitakazohusisha timu 32.
Kama atanaswa na Palmeiras atakuwa na nafasi ya kumenyana na timu ya Lionel Messi, Inter Miami ambayo imepangwa pamoja kwenye Kundi A. Lakini, pia kujiunga na Messi kwenye timu moja ni kitu kinachoweza kutokea baada ya Infantino kusema “inawezekana ikawa” wakati alipozungumzia mahali ambako Ronaldo anaweza kwenda. Gwiji huyo wa Manchester United na Real Madrid alijiunga na Al Nassr 2023 aliposaini dili alilolipwa Pauni 164 milioni kwa msimu. Kwenye kikosi Ronaldo amecheza mechi 105 na kufunga mabao 93.