Ronaldo anaweza kumpa kila Mtanzania Sh36 milioni

Muktasari:
- Kiasi hicho cha pesa kimeongezeka hivi karibuni kutokana na madili ambayo ameendelea kuyapiga licha ya umri kumtupa mkono. Ni utajiri mkubwa sana ambao kama ingekuwa ni kuugawa kwa Watanzania milioni 60, basi kila mtu angepata Sh36 milioni.
HIVI karibuni tovuti mbalimbali duniani ziliripoti kuwa utajiri wa Cristiano Ronaldo umepanda hadi kufikia dola 800 milioni ambazo ni zaidi ya Sh2 trilioni kwa pesa za Bongo.
Kiasi hicho cha pesa kimeongezeka hivi karibuni kutokana na madili ambayo ameendelea kuyapiga licha ya umri kumtupa mkono. Ni utajiri mkubwa sana ambao kama ingekuwa ni kuugawa kwa Watanzania milioni 60, basi kila mtu angepata Sh36 milioni.
Hapa tumekuelezea kwa kina jinsi staa huyu anavyozidi kuongeza utajiri wake kupitia biashara na madili mbalimbali.

ANAPIGAJE PESA
Kwa sasa, Ronaldo anachezea Al-Nassr ya Saudi Arabia, akilipwa mshahara wa takribani dola 200 milioni kwa mwaka. Hii ni pamoja na mishahara, bonasi na haki za kibiashara za picha.
Ukiondoa mshahara, Ronaldo anapata pesa nyingi sana nje ya uwanja kupitia biashara zake na mikataba ya ubalozi aliyoingia.
Kwanza ana mkataba wa maisha na kampuni ya Nike ambao una thamani ya dola 1 bilioni, Clear (shampoo), Herbalife, TAG Heuer (saa), Binance, Shopee, na Arman.
Kiujumla mikataba yote hii kwa mwaka inamwingizia zaidi ya dola 70 milioni.
Pia fundi huyu ana biashara zake kadhaa ambazo zinamwingizi pesa za kutosha, biashara hizo ni pamoja na:
CR7 Underwear: Bidhaa za nguo za ndani.
CR7 Hotels (Pestana CR7): Hoteli zenye hadhi ya juu nchini Ureno na Hispania.
CR7 Fragrances: Pafyumu
CR7 Crunch Fitness: Gym
Amekuwa pia akijipatia mkwanja wa kutosha kupitia mitandao ya kijamii ambako ana akaunti ya YouTube inayompa karibia Dola 50,000 kila mwezi, pia kwa upande wa Instagram kwa kila chapisho moja anapata Dola 3 milioni.

MSAADA KWA JAMII
Aliwahi kutoa zaidi ya Dola 1 milioni kwa hospitali za Ureno wakati wa mlipuko wa Corona, pia amekuwa akichangia sana matibabu ya watoto wanaosumbuliwa na magonjwa makubwa kama kansa.
Aliwahi kudiriki kuuza moja ya tuzo zake za Ballon d’Or kwa dola 600,000, na pesa zote alizitoa kama msaada kwa watoto wa Palestina.
Kwa sasa ni balozi wa Save the Children, UNICEF, na World Vision ambayo ni mashirika ya kusaidia jamii.

NDINGA
Bugatti Centodieci - Dola 9 milioni
Bugatti Chiron - Dola 3 milioni
Lamborghini Aventador - Dola 500,000
Ferrari F12 TDF - Dola 550,000
McLaren Senna - Dola 1 milioni
Rolls Royce Cullinan - Dola 400,000
Rolls Royce Phantom Drophead Coupe - Dola 500,000
Bentley Flying Spur - Dola 220,000
Mercedes G-Wagon Brabus - Dola 700,000
Aston Martin DB9 - Dola 200,000

MIJENGO
Anaripotiwa kuwa na nyumba nne ingawa kwa sasa akiwa huko Saudi Arabia amepanga katika mjengo ambao kwa mwezi analipa Dola 250,000.
Nyumba anazomiliki ni pamoja na ile ya Madeira, Ureno yenye thamani ya dola 8 milioni, Madrid, Hispania Dola 6 milioni, Turin, Italia, Dola 4 milioni na Manchester, Uingereza yenye thamani ya Dola 3 milioni.
MAISHA NA BATA
Ana watoto watano. Wa kwanza ni Cristiano Ronaldo Jr ambaye hivi karibuni aliitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ureno kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17.
Wengine ni Eva Maria, Mateo Ronaldo, Alana Martina dos Santos Aveiro na Bella Esmeralda dos Santos Aveiro.
Kwa sasa bado yupo katika uhusiano na mrembo Georgina Rodriguez ambaye baadhi ya ripoti zinadai tayari ameshamuoa.