Ronaldo ampokea Mane kwa keki ya ubingwa
Muktasari:
- Simba wa Teranga ilitwaa taji lao la pili la AFCON baada ya fainali yenye utata dhidi ya Morocco, wenyeji wa mashindano, mjini Rabat Jumapili.
RIYADH, SAUDI ARABIA: SUPASTAA, Cristiano Ronaldo na wachezaji wenzake wa Al-Nassr waliandaa mapokezi ya furaha kwa Sadio Mane, wakimpa keki maalumu baada ya kurejea kutoka kwenye ushindi wa kihistoria wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) akiwa na Senegal.
Simba wa Teranga ilitwaa taji lao la pili la AFCON baada ya fainali yenye utata dhidi ya Morocco, wenyeji wa mashindano, mjini Rabat Jumapili.
Mane, 33, aliiongoza Senegal kushinda 1-0 baada ya muda wa nyongeza, kufuatia bao la ushindi lililofungwa na Pape Gueye katika dakika ya 94.
Utata ulitokea baada ya Morocco kupewa penalti yenye utata mkubwa mwishoni mwa muda wa kawaida, jambo lililosababisha kikosi cha Senegal kinachoongozwa na kocha Pape Thiaw kuondoka uwanjani kwa hasira.
Lakini, gwiji huyo wa zamani wa Liverpool Mane aliwarejesha wachezaji wenzake uwanjani baada ya dakika 17 za vurugu, hatua iliyowezesha fainali hiyo kuendelea. Hatimaye, nyota wa Real Madrid, Brahim Díaz, alikosa penalti ya aina ya Panenka, akiupiga mpira moja kwa moja mikononi mwa aliyekuwa kipa wa Chelsea, Edouard Mendy, ambaye hakuhitaji hata kusogea na kuudaka mpira.
Nyota huyo wa Al-Nassr alirejea Saudi Arabia siku ya Ijumaa kuungana tena na kikosi cha Jorge Jesus. Na mshambuliaji huyo alipokelewa kwa furaha kubwa na wachezaji wenzake wote. Kamera zilimwonyesha akiwakumbatia wachezaji wa Al-Nassr kabla ya wote kukusanyika kuzunguka keki maalumu, aliyokabidhiwa na nahodha Ronaldo, 40.
Keki hiyo ilimwonyesha mchezaji huyo wa zamani wa Southampton akiwa ameshika taji la AFCON, akisherehekea pamoja na wachezaji wenzake nchini Morocco. Pia ilikuwa na maandishi: “Hongera bingwa Senegal. Hongera Sadio.”
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Senegal alikata kipande cha keki na kushangiliwa na wachezaji wenzake wa Al-Nassr.
Mané kisha alisema: “Asanteni, ndugu zangu.”