Ronaldo afunika kwa mabao duniani

Muktasari:

Bao alilofunga Ronaldo kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Supercoppa Italiana dhidi ya  Napoli  limemfanya kuwa juu ya mchezaji wa zamani wa Kimataifa wa Jamhuri ya Czech, Josef Bican, aliyekuwa na mabao 759.

TURIN, ITALIA. MSHAMBULIAJI wa Juventus, Cristiano Ronaldo  amekuwa kinara kwenye  orodha ya  wachezaji  wenye mabao mengi zaidi kwenye historia ya mchezo wa mpira wa miguu duniani, akifikisha jumla ya  mabao 760.

Ronaldo ameendelea kuonyesha ubora wake  wa kucheka na nyavu  baada ya hapo jana, Jumatano Januari 20 kuifungia bao moja kati ya mawili ya Juventus kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Supercoppa Italiana dhidi ya Napoli.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 35 na mshindi mara tano wa Ballon d'Or  amemzidi kete mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa la Brazil, Pele (757)  ambaye yupo nafasi ya tatu kwenye orodha hiyo pamoja  na Romario akiwa nafasi ya nne (743), mpinzani wa Ronaldo, Lionel Messi yupo nafasi tano (719).

Jumla ya mabao 760 yaliyorekodiwa na Opta, 450  ameyafunga wakati akiwa na Rael Madrid ndani ya miaka yake tisa aliyocheza soka la kulipwa Hispania, 118 alifunga akiwa na  Manchester United, 102 akiwa na timu yake ya taifa la Ureno  huku 85 akiwa na klabu yake ya sasa na matano akiwa na  Sporting Lisbon.

Miaka iliyokuwa na mafanikio makubwa  zaidi kwa Ronaldo upande wa upachikaji wake mabao ni 2007 (34), 2008 (35), 2009 (30), 2010 (48), 2011 (60), 2012 (63), 2013 (69) , 2014 (61), 2015 (57), 2016 (55) na 2017 (53).

Mshindi huyo mara tano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya miaka aliyokuwa na mafanikio zaidi ya kufunga mabao upande huo ni kuanzia 2011-12 anajumla ya mabao 69.

Ronaldo  amefunga mabao 27 dhidi ya Sevilla kuliko klabu nyingine lakini pia amefunga mabao 25 dhidi ya Atletico Madrid  na mabao 23 dhidi ya Getafe. Huyu bwana balaa lake ni zito, amefunga mabao 488 kwa mguu wake wa kulia na 139 kwa mguu wa kushoto huku mabao 131 yakiwa kwa kichwa.

Akiwa nyumbani na machama yake aliyoyachezea Ronaldo amefunga mabao  410 huku  304  yakiwa ugenini lakini pia amefunga mabao  46 kwenye viwanja ambavyo hapakuwa na mwenyeji, timu zote zikiwa ugenini.

Anajumla ya mabao 311 kwenye Ligi ya Hispania 'LaLiga',Ligi ya Mabingwa Ulaya (134), Ligi Kuu England (84), Ligi Kuu Italia (67), Kufuzu Kombe la dunia (30), Kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Ulaya (31), Kombe la FA (13) na saba kwenye Kombe la dunia.