Ronaldo afunga friikiki baada ya miaka tatu

RIYADH, SAUDI ARABIA. NYOTA wa Al- Nassr, Cristiano Ronaldo, amefunga bao la free-kick kwa mara ya kwanza baada miaka mitatu iliyopita akiisaidia timu yake kuibuka na ushindi.

Ronaldo aliwahi kufunga bao la free-kick ilikua dhidi ya Portsmouth kwenye mechi ya Ligi Kuu England wakati anakipiga Manchester United kabla ya kutimkia Real Madrid.

Mara ya mwisho Ronaldo kufunga bao la free-kick ilikuwa Julai mwaka 2020 kipindi anakipiga Juventus. Bao hilo alifunga dhidi ya Torino Juventus ikiibuka na ushindi wa mabao 4-1.

Sasa Ronaldo amefuta ukame wa mabao aina ya free-kick baada ya kufunga dakika ya 78 wikiendi iliyopita, yenye umbali wa mita 30. Al-Nassr ilikua nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya Abha kabla ya Ronaldo kupachika bao hilo.

Nyota huyo mara tano wa tuzo ya Ballon d'Or alikwamisha mkwaju huo wa free-kick baada ya hapo akakimbia kwa furaha akishangilia, huku akiruka juu na kuwapungia mikono mashabiki kwa kuwapigia mayowe.

Timu ya Abha ilikuwa pungufu baada ya mchezaji wao Zakaria Sami Al Sudan kulimwa kadi yekundu, lakini Al-Nassr ikaibuka na kupachika bao la pili kupitia Anderson Talisca dakika ya 86 ya mtanange huo, hiyo ni baada ya Ronaldo kusawazisha bao.

Baada ya ushindi huo Al-Nassr imeinyemelea vinara wa ligi Al-Ittihad kwa tofauti ya pointi moja tu kwenye msimamo wa ligi ya Saudi Pro, Al-Nassr ina pointi 49 wakati vinara wa ligi wana pointi 50.

Ronaldo ameendelea kufurahia maisha ndani ya jiji la Riyadh baada ya kusuasua mechi za mwanzo baada ya kujiunga na Al-Nassr.