Rodrygo aingia katika orodha ya Arne Slot

Muktasari:
- Diaz ameingia katika rada za Barcelona hivi karibuni baada ya timu hiyo kushindwa kuipata huduma ya Nico Williams aliyesaini mkataba mpya na Athletic Bilbao.
Liverpool itajiunga na Arsenal kuiwania huduma ya winga wa Real Madrid, Rodrygo, 24, ikiwa winga wa, Luis Diaz, 28, ataenda Barcelona dirisha hili.
Diaz ameingia katika rada za Barcelona hivi karibuni baada ya timu hiyo kushindwa kuipata huduma ya Nico Williams aliyesaini mkataba mpya na Athletic Bilbao.
Rodrygo anataka kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kutosha kikosi cha kwanza cha Madrid na hajioni katika mipango ya kocha Xabi Alonso msimu ujao.
Fundi huyu wa kimataifa wa Brazil anauzwa kwa kiasi kisichopungua Pauni 70 milioni na mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Arsenal imeshindwa kufikia makubaliano ya kumnunua staa huyu hadi sasa licha ya kuanza mazungumzo kwa muda mrefu kwa sababu inataka bei yake ipunguzwe.
Akiwa chini ya Carlo Ancelotti msimu ulipita, Rodrygo alicheza mechi 54 za michuano yote na kufunga mabao 14.
Kocha wa Madrid, Xabi Alonso, juzi baada ya mechi alipoulizwa ikiwa ni kweli Rodrygo kuwa katika mipango ya kuuzwa hakuweka wazi juu ya suala hilo.
Liverpool ina matumaini makubwa ya kumpata Rodrygo kutokana na mahusiano yao na Madrid waliyoyajenga hivi karibuni hususani baada ya kuwauzia Trent Alexander Arnold.
Alejandro Garnacho
NAPOLI imerejea tena katika harakati za kumsajili winga wa Manchester United na timu ya taifa ya Argentina, Alejandro Garnacho, mwenye umri wa miaka 21, katika dirisha hili la majira ya kiangazi. Mabosi wa Napoli wana matumaini ya kuipata huduma ya fundi huyu kwa kiasi kisichozidi Pauni 45 milioni. Garnacho hayuko katika mipango ya Kocha wa Man United, Ruben Amorim na ameambiwa atafute mahala pa kwenda kucheza msimu ujao.
Bryan Mbeumo
MANCHESTER United bado ina matumaini ya kukamilisha dili la kumsaini mshambuliaji wa Brentford na timu ya taifa ya Cameroon, Bryan Mbeumo, mwenye umri wa miaka 25, kabla ya kuanza ziara yao ya maandalizi ya msimu mpya huko Marekani. Mkataba wa Mbeumo unatarajiwa kumalizika mwaka 2026, na yeye mwenyewe yupo tayari kujiunga nao katika dirisha hili kwani ameshafanya hadi makubaliano nao binafsi.
Sean Longstaff
NEWCASTLE United imekataa ombi la tatu kutoka Leeds United la kumuuza kiungo wao raia wa England, Sean Longstaff, mwenye miaka 27, dirisha hili la majira ya kiangazi. Sean ni miongoni mwa mastaa ambao hawapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Newcastle na inadaiwa yuko tayari kuondoka ili kwenda kupata timu itakayomfanya aonyeshe kiwango chake na Leeds inaona ni mtu sahihi kwao.
Rodolfo Aloko
ASTON Villa na Brighton zinamfuatilia kiungo mshambuliaji chipukizi kutoka Benin, Rodolfo Aloko, mwenye umri wa miaka 18, anayekipiga katika timu ya NK Kustosija ya Croatia. Aloko ni miongoni mwa makinda wanaofanya vizuri kwa sasa huko Croatia na msimu uliopita alionyesha kiwango kizuri katika mechi tofauti alizocheza na kuzivutia baadhi ya timu za Ligi Kuu England zikiwamo hizo mbili.
Andre Onana
MANCHESTER United huenda ikashusha bei yao ta Pauni 30 milioni dirisha hili kwa ajili ya kumuuza kipa wake, Andre Onana. Taarifa mbalimbali zinadai AS Monco inatamani sana huduma ya fundi huyu lakini kiasi hicho cha pesa kinachotajika na Man United kama ada ya uhamisho ni kikubwa sana kwao. Kipa huyu wa kimataifa wa Cameroon anahusishwa kuondoka kutokana na kiwango chake.
Matt O’Riley
AS Roma inataka kumsajili kiungo wa kati wa Brighton na timu ya taifa ya Denmark, Matt O’Riley, 24, katika dirisha hili la majira ya kiangazi. Benchi la ufundi la Roma limevutiwa sana na kiwango alichoonyesha staa huyu msimu uliopitana alicheza mechi 26 za michuano yote. Kuna kila dalili nyota huyo akahamia Ligi Kuu ya Italia msimu ujao.
Jadon Sancho
HATIMAYE ripoti zinaeleza Manchester United ipo tayari kupunguza bei ya winga wao raia wa England, Jadon Sancho, mwenye umri wa miaka 25, ili kumuuza dirisha hili la majira ya kiangazi. Timu nyingi zimekuwa zikirudi nyuma katika dili la staa huyo kutokana na bei yake jambo ambalo linazidi kuchelewesha mchakato wa kumuuza.