Robbie Keane kupewa kimeo Spurs
Muktasari:
- Klabu hiyo inayojulikana kama Lilywhites kwa sasa iko katika mapambano makali ya kubaki kwenye Ligi Kuu England baada ya kukosa ushindi kwa muda mrefu, hali iliyowaacha pointi moja tu juu ya eneo la kushuka daraja.
LONDON, ENGLAND: TOTTENHAM Hotspur inaripotiwa kumfikiria Robbie Keane kama kocha mpya kwa ajili ya msimu ujao huku ikijaribu kukabiliana na kipindi kigumu zaidi katika historia ya hivi karibuni ya klabu hiyo.
Klabu hiyo inayojulikana kama Lilywhites kwa sasa iko katika mapambano makali ya kubaki kwenye Ligi Kuu England baada ya kukosa ushindi kwa muda mrefu, hali iliyowaacha pointi moja tu juu ya eneo la kushuka daraja.
Kocha wa muda, Igor Tudor hatarajiwi kuendelea na nafasi hiyo kwa kudumu baada ya msimu wa 2025–26 kumalizika, bila kujali kama klabu itabaki kwenye ligi kuu au la.
Ingawa uongozi wa klabu unaaminika umetambua majina kadhaa makubwa kwa ajili ya kuongoza ujenzi upya wa timu, kutokuwa na uhakika kuhusu kama watabaki kwenye Ligi Kuu kumeifanya kazi ya kupata kocha mpya kuwa ngumu zaidi.
Kwa mujibu wa ripoti ya GiveMeSport, mshambuliaji wa zamani wa Spurs, Keane, ameibuka kama mgombea anayeweza kupewa nafasi ya ukocha msimu huu wa joto. Keane mwenye umri wa miaka 45 kwa sasa anaiongoza klabu kubwa ya Hungary, Ferencvárosi TC na amedumisha kiwango kizuri cha ushindi cha asilimia 61 na pia ameshinda ubingwa wa ligi ya ndani.
Ingawa Mauricio Pochettino na Roberto De Zerbi bado ni malengo makuu ya viongozi wa klabu, Keane anaonekana kama mbadala muhimu iwapo Spurs watashindwa kuwapata makocha hao wanaowapendelea. Inaelezwa Keane atakuwa chaguo pekee la timu hiyo endapo kama itashuka daraja na kwenda kucheza kwenye Championship msimu ujao.