Baada ya kukiwasha dhidi ya Spurs, Arteta afichua hasira za Eze
Muktasari:
- Arteta amezungumza na vyombo vya habari baada ya Eze kufunga mabao mawili katika ushindi wa 4-1 iloupata Arsenal dhidi ya Tottenham Hotspur, jana Jumapili usiku.
KOCHA Mkuu wa Arsenal, Mikel Arteta, amedai kuwa kiungo Eberechi Eze, alikuwa na hisia za kukasirishwa na hatua ya kucheza mechi chache hivi karibuni.
Arteta amezungumza na vyombo vya habari baada ya Eze kufunga mabao mawili katika ushindi wa 4-1 iloupata Arsenal dhidi ya Tottenham Hotspur, jana Jumapili usiku.
Ushindi huo umewawezesha The Gunners kurekebisha nafasi yao na kuongoza Ligi Kuu ya England kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Manchester City.
Arteta alimpa Eze nafasi ya kuanza katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Tottenham Hotspur, hali iliyompa mchezaji huyo fursa ya kufunga bao mapema katika kila nusu ya mechi.
“Ninaweza kuona alikuwa anataka kuthibitisha kitu. Alinikasirikia hata na mimi, kwa sababu sikumchezesha siku zilizopita. Sasa ninaanza kuelewa jinsi ya kumtumia na kukiwezesha kiwango chake kuwa bora zaidi," amesema Arteta.
Hata hivyo, kocha huyo amesema, uhusiano wake na Eze unaendelea kuimarika, huku akisisitiza kufahamu namna ya kutumia uwezo wa kipekee wa mchezaji huyo katika mechi zijazo za Arsenal.
Katika mechi ya jana dhidi ya Spurs iliyokubali kichapo cha 4-1, mabao ya Arsenal yalifungwa na Eberechi Eze (dakika ya 32 na 61) na Viktor Gyökeres (dakika ya 47 na 90+7). Bao la Tottenham lilifungwa na Randal Kolo Muani dakika ya 34.
Baada ya ushindi huo, Arsenal imeendelea kuwa kinara kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England, huku ikikusanya pointi 61 kutoka mechi 28, na kuongoza kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Manchester City yenye mechi moja mkononi.
Tottenham iko nafasi ya 16 katika jedwali la ligi huku ikiwa na pointi 29, na kukaribia maeneo ya kushuka daraja.
Arsenal sasa ina ratiba ndefu ya mechi za ligi zinazobaki msimu huu. Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu ya England kwa msimu wa 2025-2026.
Baadhi ya mechi zilizobaki kwa Arsenal ambazo ni muhimu sana kushinda katika kampeni ya kukuza nafasi ya ubingwa kwa timu hiyo, hasa dhidi ya Manchester City inayoweza kuamua hatima ya taji la Ligi Kuu msimu huu, ni kama ifuatavyo:
Arsenal vs Chelsea (nyumbani)
Brighton vs Arsenal (ugenini)
Arsenal vs Everton (nyumbani)
Bournemouth vs Arsenal (ugenini)
Manchester City vs Arsenal (ugenini)
Arsenal vs Newcastle (nyumbani)
Arsenal vs Fulham (nyumbani)
West Ham vs Arsenal (ugenini)
Arsenal vs Burnley (nyumbani)
Crystal Palace vs Arsenal (ugenini)