Gwiji Spurs amwonya kocha Igor Tudor
Muktasari:
- Tudor, 47, alirithi mikoba ya kocha wa zamani wa Spurs, Thomas Frank, Ijumaa iliyopita baada ya kusaini mkataba wa muda mfupi hadi mwisho wa msimu.
LONDON, ENGLAND: GWIJI wa Tottenham Hotspur, Tim Sherwood, amemwonya kocha mpya wa mpito Igor Tudor kwamba kuna hasara kubwa na faida ndogo sana katika kazi yake mpya ya kuinoa miamba hiyo ya London.
Tudor, 47, alirithi mikoba ya kocha wa zamani wa Spurs, Thomas Frank, Ijumaa iliyopita baada ya kusaini mkataba wa muda mfupi hadi mwisho wa msimu.
Mengi yamesemwa kuhusu uteuzi huo na Sherwood, 57, alidokeza kuwa fundi huyo wa Croatia huenda amejiingiza katika hali isiyo na ushindi wowote kwani anaweza tu kushindwa. Nyota huyo wa zamani wa Spurs na kocha pia, ambaye hivi karibuni alikiri kuwa “itakuwa heshima” kurejea klabuni hapo baada ya Frank kuondolewa Jumatano, alizungumzia hatari ya timu hiyo kushuka daraja katika Ligi Kuu.
Klabu hiyo ya Kaskazini mwa London ipo nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na tofauti ya alama tano tu kutoka eneo la kushuka daraja. Sherwood anasisitiza kuwa kama Tudor atashindwa kuiokoa Spurs, basi taaluma yake itaathirika milele kama mtu aliyeshusha daraja moja ya klabu za Big Six.
Hata hivyo, gwiji huyo wa Blackburn Rovers aliongeza kuwa hata kama kocha huyo wa zamani wa Juventus ataiokoa klabu hiyo kwenye sakata la kushuka daraja na kumaliza katika nafasi za juu zaidi, bado hatapewa sifa yoyote. Hiyo ni kwa sababu ya kikosi chenye majina makubwa cha Tottenham, licha ya ukweli kwamba wachezaji 11 kwa sasa wapo majeruhi.
Sherwood aliiambia Sky Sports: "Itakuwa vigumu, hana uzoefu wa Ligi Kuu England. Mbali na fedha, faida yake ni nini? Kama atamaliza nafasi ya 12, hatapewa sifa yoyote. Hasara inaweza kuwa kubwa mno. Je, ungependa jina lako lihusishwe na Tottenham kushuka daraja kutoka Ligi Kuu? Ninarudia, Thomas Frank angekuwa bado yupo kama si hali ya sumu kutoka kwa mashabiki.
“Na ninaelewa kabisa kutoridhika kwa mashabiki kwa sababu hawapati matokeo. Nimesikia watu wakisema wanatembea usingizini kuelekea Championship. Nafikiri watakuwa na uwezo wa kujinasua, hata wakiwa na majeraha, lakini hatapewa sifa kwa hilo. Hasara ni kubwa sana, anaweza tu kushindwa. Hatapewa sifa kwa kuinusuru Tottenham kwenye ligi.”