Ripoti yaipa penalti Everton kwa Arsenal
Muktasari:
- Katika mechi hiyo iliyopigwa Desemba 20, kwenye dimba la Hill Dickinson, kulikuwa na tukio la beki wa Arsenal William Saliba kumchezea vibaya katika boski staa wa Everton, Thierno Barry wakati wanagombania mpira.
LONDON, ENGLAND: RIPOTI kutoka Jopo la uchunguzi wa matukio tata katika mechi za Ligi Kuu England imefichua kuwa Everton ilipaswa kupewa faida ya pigo la penalti katika mechi yao dhidi ya Arsenal iliyomalizika kwa kupoteza kwa bao 1-0.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Desemba 20, kwenye dimba la Hill Dickinson, kulikuwa na tukio la beki wa Arsenal William Saliba kumchezea vibaya katika boski staa wa Everton, Thierno Barry wakati wanagombania mpira.
Katika mchezo huo uliomshuhudia kocha wa Arsenal Mikel Arteta akikutana tena na meneja wa Everton David Moyes aliyemfundisha wakati wa enzi zake za uchezaji, Arsenal ilipata bao la kuongoza baada ya Viktor Gyokeres kufunga penalti, iliyotokana na Jake O’Brien kushika mpira ndani ya eneo la boski.
Hata hivyo, Everton walihisi walipaswa pia kupewa penalti baada ya tukio lililohusisha Saliba na Barry wakati pale mchezo ulipokaribia dakika ya 60.
Ripoti inaeleza, wachezaji hao wawili walipokutana ndani ya boksi, Barry alikuwa ameufikia mpira kabla ya Saliba, ambaye alimkanyaga kiatu mshambuliaji huyo wa Toffees na kumwangusha chini.
Hata hivyo, mwamuzi Sam Barrott alikataa kwenda kutazama marejeo ya video, na Mwamuzi Msaidizi wa Video (VAR) hakumshauri kwenda kufanya hivyo kwa kile kilichoelezwa kuwa mguso wa Saliba kwa Barry haukuwa wa kutosha kiasi cha Everton kupewa penalti.
Jopo la uchunguzi wa matukio tata katika mechi za Ligi Kuu England huundwa na wajumbe watano ambao ni wachezaji au makocha wa zamani watatu, mwakilishi mmoja kutoka Ligi Kuu England na mmoja kutoka kamati ya kusimamia waamuzi yaani Professional Game Match Officials Limited (PGMOL).
Arsenal ilifanikiwa kuondoka na pointi zote tatu katika Uwanja wa Hill Dickinson, matokeo ambayo kwa wakati huo yaliifanya kuwa mbele kwa pointi mbili dhidi ya wapinzani wao wa mbio za ubingwa, Manchester City.
Vijana hao wa Arteta kutoka kaskazini mwa London, wanawania kutwaa taji lao la kwanza la ligi tangu msimu wa 2003-04, na kwa sasa wako mbele kwa pointi tano dhidi ya Man City kufuatia ushindi wao wa mabao 4-1 dhidi ya Aston Villa Jumanne.