Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ghafla ubingwa wa Ligi Kuu England hugeuka mbio za farasi watatu

UBINGWA Pict

Muktasari:

  • Ushindi wote ulikuwa kwa matokeo ya 2-1; Arsenal iliichapa Brighton, Manchester City iliitandika kwa shida Nottingham Forest, huku Aston Villa wakipindua mechi na kushinda ugenini dhidi ya Chelsea.

LONDON, ENGLAND: Na timu zote tatu zinazowania ubingwa wa Ligi Kuu England zilishinda mechi zao Jumamosi, na hali ikaendelea kubaki kama ilivyokuwa.

Ushindi wote ulikuwa kwa matokeo ya 2-1; Arsenal iliichapa Brighton, Manchester City iliitandika kwa shida Nottingham Forest, huku Aston Villa wakipindua mechi na kushinda ugenini dhidi ya Chelsea.

Baada ya michezo 18, kikosi cha Mikel Arteta kinaendelea kuongoza ligi kikiwa na pointi 42. Man City iko nyuma kwa pointi mbili, huku Aston Villa wakiwa nyuma kwa pointi tatu tu.

Hali ni tete sana na kuongeza msisimko, Kocha Unai Emery ataiongoza Aston Villa kuikabili Arsenal kwenye Uwanja wa Emirates siku ya Jumanne.

Emery tayari aliwapa klabu yake ya zamani moja ya vipigo viwili vyao msimu huu, huku Emi Buendía akifunga bao la ushindi dakika za mwisho huko Midlands Magharibi, na haikuwa mara ya kwanza kwa Emery kuwaumiza waajiri wake wa zamani.

Msimu bado ni mrefu, na mzunguko ujao wa mechi hautaamua hatima ya ubingwa moja kwa moja. Zaidi ya hayo, dirisha la usajili linafunguliwa siku mbili tu baada ya Arsenal kuwakaribisha Aston Villa, huku klabu zote mbili pamoja na wapinzani wao Man City zitakuwa na maamuzi muhimu ya kufanya kuhusu vikosi vyao.

Kwa hiyo, ni mambo gani muhimu ya kuangalia katika vita vya ubingwa? Makala haya yanajaribu kuchambua uhondo kamili.


UBIN 02

Pointi muhimu mechi kubwa

Arsenal haikuwa katika kiwango chao bora ilipocheza Villa Park mwanzoni mwa Desemba, lakini bado walikaribia kupata sare. Bao lao la kusawazisha lilikuja katika kipindi kifupi cha ubora baada ya Leandro Trossard kuingia kutoka benchini, lakini Aston Villa walirejea na kupata ushindi katika dakika za mwisho.

Kikosi cha Mikel Arteta kimekuwa kikishiriki mbio za ubingwa katika misimu mitatu iliyopita, na mechi dhidi ya Aston Villa zimekuwa na uzito mkubwa mara kadhaa. Ushindi wa kusisimua wa 4-2 mwaka 2023 ulionekana kama tamko la kweli la ubingwa kwa Arsenal, lakini mbio hizo zilisambaratika mwishoni mwa msimu.

Kipigo cha Aprili 2024 na kupoteza uongozi wa mabao 2-0 Januari 2025 pia viliumiza klabu hiyo ya London kwa namna tofauti. Jambo muhimu kwa Arsenal safari hii linaweza kuwa kurejea kwa beki Gabriel. Mbrazili huyo aliingia kama mchezaji wa akiba katika ushindi wa Jumamosi dhidi ya Brighton baada ya kukosa mechi sita za ligi kutokana na jeraha alilopata akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Brazil. Alikosa pia mechi ya kwanza dhidi ya Aston Villa.


UBIN 03

Uamuzi wa Januari

Timu zote tatu zimefaidika na usajili wa mwezi Januari katika misimu ya hivi karibuni. Trossard, Jorginho na Jakub Kiwior waliiongezea Arsenal kina mwaka 2023, huku Man City wakisajili wachezaji kama Omar Marmoush na Nico González katika matumizi ya Pauni 200 milioni kwenye dirisha Januari 2025.

Aston Villa pia ilikuwa bize ikifanya usajili wa mkopo wa Marco Asensio na Marcus Rashford, jambo lililofuatiwa na mfululizo wa pointi 29 katika mechi 14 na kuwafanya wakose kwa karibu kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hata hivyo, huenda si wao pekee watakaokuwa kwenye hekaheka za usajili katika dirisha la Januari 2026.

Swali kubwa linamhusu Antoine Semenyo ambaye inaripotiwa anataka kujiunga na Man City. Itagharimu Pauni 65 milioni kumsajili mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ghana, lakini angekuwa chaguo la haraka kutumika na huenda akaleta tofauti katika mbio za ubingwa.

Arsenal pia haijakataa uwezekano wa kuwekeza zaidi, huku msimu uliopita ukiwa si Januari pekee yenye usajili mkubwa kwa Aston Villa. Nyota Morgan Rogers alijiunga kutoka Middlesbrough katikati ya msimu wa 2023/24, wakati Jhon Duran alikuwa usajili wa gharama kubwa wa Januari katika msimu wa kwanza wa Emery huko Villa Park.

Aston Villa huenda wakahisi wanahitaji mshambuliaji mwingine, licha ya Ollie Watkins kufunga mabao mawili ya ushindi dhidi ya Chelsea Jumamosi. Watkins na Donyell Malen wana jumla ya mabao tisa tu ya ligi, huku jumla ya mabao 29 ya Aston Villa ikiwa ya chini zaidi miongoni mwa timu sita bora kwa sasa.


UBIN 01

Majeraha Hutibua mipango

Arsenal ilikosa huduma za Jurrien Timber na Riccardo Calafiori dhidi ya Brighton Jumamosi, huku Ben White na Cristhian Mosquera pia wakiwa nje, hali iliyowaacha na safu ya ulinzi iliyo dhaifu.

Kai Havertz yuko karibu kurejea, huku kiwango cha Gabriel Jesus tangu alipopona jeraha la muda mrefu kikimfurahisha Arteta. “Nadhani Gabriel ana mengi ya kuipa timu, na amethibitisha hilo mara moja alipokuwa tayari kucheza,” alisema kocha huyo akionekana kuondoa uwezekano wa mchezaji huyo kuondoka Januari.

Man City inawakosa Omar Marmoush na Rayan Aït-Nouri kwa kipindi chote ambacho nchi zao zitakuwa kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), ingawa John Stones na Jeremy Doku wanaweza kurejea mapema baada ya majeraha. Aston Villa nao wanawakosa wachezaji kadhaa, akiwemo Evann Guessand aliyeitwa AFCON dakika za mwisho.

Kwa timu zote tatu, si suala la nani hayupo tu, bali ni jinsi watakavyokabiliana na hali hiyo. Msimu uliopita, Arsenal walionekana kuchoka mwishoni baada ya majeraha ya Havertz na Gabriel Jesus kuwaacha na chaguo chache sana mbele, na sasa watataka kuepuka kurudia hali hiyo.


Mechi tano zijazo

Arsenal na Aston Villa huenda hawataangalia zaidi ya mechi yao kwa sasa, lakini ratiba inayofuata ina changamoto nyingi. Arsenal itawakabili Bournemouth (ugenini), Liverpool (nyumbani), Nottingham Forest (ugenini) na Manchester United (nyumbani), na huenda wakafurahia kucheza na Liverpool wakati mabingwa hao wakiwa bila Mo Salah na Alexander Isak.

Mechi inayofuata ya Man City ni ugenini dhidi ya Sunderland, ambao wamepungukiwa na wachezaji kutokana na AFCON, kisha watawakaribisha Chelsea, Brighton, kwenda Old Trafford kukutana na Man United, na baadaye Wolves nyumbani. Derby ya Manchester inatarajiwa kuwa muhimu sana, hasa kutokana na dalili chanya za hivi karibuni za Man United.

Kwa upande wa Aston Villa, ushindi dhidi ya Arsenal huenda ukaongeza umakini kwa mechi zitakazofuata. Watacheza dhidi ya Nottingham Forest (nyumbani), Crystal Palace (ugenini), Everton (nyumbani) na Newcastle (ugenini), mechi ambazo walipata jumla ya pointi sita tu msimu uliopita. Mambo ni moto.