Rio: Huyu Mbeumo ni kama mzaha tu!
Muktasari:
- Mbeumo alijihakikishia nafasi katika kikosi cha Ruben Amorim haraka sana katika nusu ya kwanza ya msimu wa 2025/26, akifunga mabao matano katika mechi 11 za Ligi Kuu alizocheza hadi sasa.
LONDON, ENGLAND: GWIJI wa Manchester United, Rio Ferdinand amemtaja nyota wa Cameroon, Bryan Mbeumo kama 'mzaha' (yaani mchezaji wa ajabu sana) kutokana na mwanzo wake wenye ushawishi katika maisha mapya Old Trafford.
Mbeumo alijihakikishia nafasi katika kikosi cha Ruben Amorim haraka sana katika nusu ya kwanza ya msimu wa 2025/26, akifunga mabao matano katika mechi 11 za Ligi Kuu alizocheza hadi sasa.
Kulingana na Ferdinand, Mbeumo anaweza kuwa mmoja wa winga kamili zaidi katika Ligi Kuu msimu huu.
“Mbeumo amekuwa kama mzaha. Ameingia pale na kuwa mchezaji wa kudumu,” Ferdinand alisema kwa mujibu wa The Standard.
“Ni mtu anayeweza kukupa sekunde mbili au tatu akiwa na mpira ili kupunguza presha. Anaweza kufunga mabao muhimu na kutengeneza nafasi.
“Nimesikia maoni ya Thomas Frank kumhusu hivi karibuni akisema Mbeumo karibu anakuwa winga kamili.
“Nadhani kufikia mwisho wa msimu huu, atakuwa mmoja wa winga kamili zaidi katika Ligi Kuu kwa sababu anaweza kufanya kila kitu. Anachohitaji ni kufanya hivyo kwa uthabiti akiwa kwenye jezi ya United.”
Nyota huyo wikiendi iliyopita alifunga bao dhidi ya Tottenham Spurs katika mechi ya Ligi Kuu ya England iliyoisha kwa sare ya 2-2, kabla ya usiku wa jana kuwa miongoni mwa wachezaji wa Cameroon kilicholazwa bao 1-0 na DR Congo katika mechi ya nusu fainali ya play-off ya kuwania kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazochezwa nchi za Marekani, Mexico na Canada.