Mbeumo ajiweka kando ishu ya Afcon
Muktasari:
- Mbeumo, ambaye alijiunga na Man United kutoka Brentford kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi kwa ada ya Pauni 65 milioni, amezoea kwa haraka mazingira ya Old Trafford na kuonyesha ubora mkubwa ndani ya uwanja.
MANCHESTER, ENGLAND: BRYAN Mbeumo ameamua kuziachia Manchester United na Cameroon kuamua hatima yake ya kuitwa kwenye kikosi cha Afcon ili kuepusha malumbano yoyote yanayoweza kutokea baina ya pande hizo mbili.
Mbeumo, ambaye alijiunga na Man United kutoka Brentford kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi kwa ada ya Pauni 65 milioni, amezoea kwa haraka mazingira ya Old Trafford na kuonyesha ubora mkubwa ndani ya uwanja.
Mbeumo amefunga mabao manne katika mechi 10 za kwanza alizochezea Man United kwenye Ligi Kuu England na kukifanya kikosi hicho cha Ruben Amorim kuwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri msimu huu.
Alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu England kwa mwezi Oktoba.
Hata hivyo, Cameroon inakabiliwa na mechi muhimu ya mchujo wa kufuzu Kombe la Dunia 2026 huku Mbeumo akitarajiwa kwenda kucheza mechi hiyo, kabla ya kuungana tena na timu yake kwa ajili ya michuano ya Afcon, ambayo itaanza Desemba 21.
Kinachoelezwa ni kwamba Mbeumo atapenda kwenda kulitumikia taifa lake kwenye michuano hiyo, lakini atahitaji klabu yake na timu ya taifa kufikia makubaliano juu ya wakati gani wa kuruhusiwa kwenda kujiunga na kikosi cha Simba Wasioshindika.
Kwa mujibu wa kanuni za michuano ya kimataifa ya Fifa, klabu zinapaswa kuwaruhusu wachezaji wao kwenda kujiunga na timu zao za taifa wiki mbili kabla ya kuanza kwa mashindano hayo makubwa ili kutoa nafasi ya maandalizi.
Kama Man United itafuata utaratibu huo, watakwenda kukosa huduma za mastaa wake watatu, Mbeumo, Noussair Mazraou na Amad Diallo kwa muda unaokaribia wiki sita.
Man United itakabiliana na Wolves, Desemba 8, siku ambayo Cameroon inatarajia kuanza kambi yake ya kujiandaa na michuano ya Afcon. Na kinachoelezwa, Man United inatarajia kukiomba chama cha soka cha Cameroon, kinachoongozwa na Samuel Eto’o, kumruhusu Mbeumo kubaki England hadi itakapokipiga na Bournemouth, Desemba 13 na Aston Villa, Desemba 21, siku ambayo michuano ya Afcon itaanza rasmi.
Taarifa za kutoka Cameroon zimefichua kwamba maofisa wa soka la nchi hiyo wapo tayari kuzungumza na wachezaji juu ya lini wanahitaji kujiunga na timu wakati watakapokutana wiki ijayo huko Morocco kwa ajili ya mechi ya mchujo wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia.
Kwenye fainali za Afcon, Man United itakosa huduma ya mastaa wake watatu muhimu sana kikosini, Amad, atakayeenda kuitumikia Ivory Coast, Mazraoui ataenda Morocco na Mbeumo, ambaye atakuwa kwenye kikosi cha Cameroon.