Rice: Nilikasirika sana kuikosa Aston Villa
Muktasari:
- Kiungo huyo wa kimataifa wa England alirudi uwanjani na kufunga mabao mawili dhidi ya Bournemouth na kuiwezesha Arsenal kurudi kileleni mwa Ligi Kuu England.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO wa Arsenal, Declan Rice amekiri kuwa alikuwa “amekasirika sana” baada ya kukosa kucheza mechi ya timu yake dhidi ya Aston Villa kutokana na jeraha la goti.
Kiungo huyo wa kimataifa wa England alirudi uwanjani na kufunga mabao mawili dhidi ya Bournemouth na kuiwezesha Arsenal kurudi kileleni mwa Ligi Kuu England.
Katika mchezo huo uliomalizika kwa Arsenal kushinda mabao 3-2, Arsenal ndio ilikuwa ya kwanza kuruhusu bao kwa boko la Gabriel kabla ya beki huyo wa kati mwenyewe kusawazisha kisha Rice akaweka bao la pili na la tatu.
Klabu hiyo ya kaskazini mwa London sasa iko pointi sita mbele ya Aston Villa, walioko nafasi ya pili, kabla ya mchezo wa Man City na Chelsea.
Baada ya ushindi huo, Rice amesema: "Ni ushindi mkubwa. Huu ni uwanja mgumu sana kupata matokeo, tulipoteza hapa msimu uliopita. Tulipata wakati mgumu pia msimu mmoja kabla ya huo, hivyo tulijua tulichokuwa tunakikabili leo. Kocha alitueleza vizuri kuhusu hilo baada ya kuanza vibaya mechi, tulifanikiwa kurudi na kupata matokeo. Kushinda 3-2 ilikuwa matokeo makubwa sana."
Aliongeza: "Lakini kukosa kwangu mechi dhidi ya Villa kulinitia hasira sana, kurudi leo na kuisaidia timu na kufunga mabao mawili, nadhani mashabiki watakuwa wameridhika sana. Na mimi mwenyewe nina furaha kwamba nimeweza kusaidia."
Rice pia alimpongeza Martin Odegaard baada ya kumsaidia kufunga, akisema: "Ni mchezaji mzuri sana, hakuna wachezaji wengi duniani wanaoweza kupiga pasi kama yeye."
Katika mwezi huu, Arsenal itacheza mechi kubwa za ligi dhidi ya Nottingham Forest na Manchester United.